1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yatupilia mbali taarifa za Wikileaks

30 Novemba 2010

Licha ya mtandao wa WikiLeaks kusema majirani wa Kiarabu wa Iran wanaishinikiza Marekani iivamie nchi hiyo kijeshi, Iran yenyewe inasema huo ni uzushi unaowachonganisha majirani wa Uajemi na Mashariki ya Kati

https://p.dw.com/p/QLeq
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Rodham Clinton, akitoa taarifa ya serikali yake juu ya nyaraka za siri zilizochapishwa na mtandao wa Wikileaks, Jumatatu ya 29 Novemba 2010, jijini Washington. (Picha ya AP/Evan Vucci)
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Rodham Clinton, akitoa taarifa ya serikali yake juu ya nyaraka za siri zilizochapishwa na mtandao wa Wikileaks, Jumatatu ya 29 Novemba 2010, jijini Washington. (Picha ya AP/Evan Vucci)Picha: AP

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, hakukosea aliposema kwamba, uvujishaji huu wa taarifa za kidiplomasia na kijasusi uliofanywa na WikiLeaks, ungeliathiri sekta nyingi katika mahusiano ya kimataifa ulimwenguni.

Jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa uvujishaji huu sio tu kwamba ni mashambulizi dhidi ya siasa ya nje za Marekani, bali pia ni mashambuizi dhidi ya jumuiya nzima ya kimataifa, washirika, wadau, na mazungumzo ya kutafuta amani, "ambayo yanazingatia usalama wa ulimwengu mzima na kuendeleza ustawi wa uchumi."

Lakini Iran, ambayo imetajwa kwenye nyaraka za WikiLeaks kwamba imekaliwa vibaya na majirani zake wa Kiarabu, na ambavyo kwa hivyo ingelitarajiwa ije juu kwa hasira na kwa kujihami, imeonekana tafauti, na badala yake imeulaumu mtandao huo kwamba umetega mtego wa makusudi wa kuichonganisha nchi hiyo na majirani zake.

Mwanzilishi wa WikiLeaks website, Julian Assange
Mwanzilishi wa WikiLeaks website, Julian AssangePicha: AP

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, Ramin Mehmanparast, ameuambia mkutano wa waandishi wa habari hivi leo (30 Novemba 2010) mjini Tehran, kwamba kilichoonekana kwenye taarifa hizi za WikiLeaks ni njama ya makusudi.

"WikiLeaks wamepandikiza uhalifu wa Kimarekani na wa Kimagharibi ndani yake ili kuonesha kwamba ni taarifa za kweli. Maadui wa ulimwengu wa Kiislam wanatumia mradi wa kupandikiza woga dhidi ya Iran na kujenga mfarakano miongoni mwetu. Mradi huo unalinda maslahi ya utawala wa Kizayuni na marafiki zao."

Mehmanparast ameziomba nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati zisikubali kunasa katika mtego huu na zioneshe kwa vitendo kwamba njama hizi hazitazaa matunda kwa kuongeza ushirikiano na imani baina yao, badala ya utengano na kutiliana shaka.

Kauli hii inatanguliwa na ile Rais Mahmoud Ahmadinejad hapo jana, ambapo aliziita taarifa hizi kama zisizokuwa na maana na zilizojaa upotofu, huku akiahidi kwamba kamwe hazitaathiri mahusiano baina ya nchi yake na majirani zake wa Kiarabu.

Kwa vyovyote vile, nyaraka hizi za WikiLeaks zinatarajiwa kuzaa mengi kwenye ulimwengu wa diplomasia ya kimataifa na ujasusi. Hivi sasa, masuala yalilotawala kwenye medani hii, ni ikiwa kweli kunaweza kuwa na siri tena duniani, na inakuwaje siri kubwa za mataifa makubwa zinapatikana kirahisi na kusambazwa kote ulimwenguni!

John Kornblum, ambaye ni mwanadiplomasia wa Washington mjini Berlin, anasema kuwa jamii za Kimagharibi hazina tabia ya kuficha siri.

"Sababu kwa nini mwanadiplomasia anapendelea kufanya kazi hapa Berlin ni kwa kuwa Wajerumani ni wazungumzaji sana. Mtu anaweza kwa haraka kukipata akitakacho kwa kujaribu tu kuwa rafiki. Na kwa kusikia tu, mtu anaweza kusikia mengi, mengi tu. Kwa miaka mingi nimezisikia siri zisisohisabika."

Na ni siri hizi zisizohisabika ndizo ambazo sasa zinaishambulia si Marekani tu, bali ulimwengu mzima, mithali ya vile mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 2001 yalivyoitikisa dunia yote.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Bergmann, Christian/AFPE

Mhariri: Othman Miraj