1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yawekewa vikwazo

Mwakideu, Alex4 Machi 2008

Huku baraza la usalama la umoja wa mataifa likiwekea vikwazo Iran inasisitiza kwamba vikwazo hivyo vinakwenda kinyume na sheria za kimataifa

https://p.dw.com/p/DHn5
Balozi wa Iran kwa Umoja wa Mataifa Mohammad Khazee akihutubia wanachama wa baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: AP

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeiwekea vikwazo Iran kwa kukataa kusitisha mpango wake wa nyuklia na maswala mengine yanayotishia usalama duniani.

Wakati nchi mbali mbali zikiendelea kuunga mkono vikwazo hivyo Iran imesisitiza kwamba vinakwenda kinyume na sheria.

Kulikuwa na kura 14 zilizopigwa kuunga mkono vikwazo dhidi ya Iran. Indonesia ndio nchi ya pekee ambayo haikushiriki katika kura hiyo.

Hata hivyo balozi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa Marty Natalegawa alieleza sababu za kutoshiriki katika kura hiyo.

Awali disemba mwaka wa 2006 na March mwaka wa 2007 azimio lengine la kuiwekea vikwazo Iran lilipasishwa bila kupingwa lakini wajumbe katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamesema vikwazo vilivyotolewa jana vimepitisha ujumbe wa maana zaidi kwa Iran.

Hata hivyo Iran ilipuuza vikwazo vya awali na pia vya sasa ikisema kwamba vinakiuka sheria za kimataifa na kwamba vinaathiri tu misimamo ya mataifa 15 yanayojumuisha baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Vikwazo vya sasa vinawanyima baadhi ya viongozi na makampuni nchini Iran usafiri na pia kuzikandamiza njia zao za kifedha.

Vile vile vinasisitiza zaidi vikwazo vya zamani kuhusu ya biashara ya bidhaa zinazotumika na wananchi pamoja na wanajeshi.

Kabla ya kura Balozi wa Iran kwa Umoja wa Mataifa Mohammad Khazee aliliambia baraza la Usalama la Umoja wa huo kwamba haliwezi kuaminika tena akidai limekuwa likitumika kutekeleza matakwa ya nchi chache.

Vile vile alipuuza ripoti mpya ya upelelezi kutoka Marekani inayosema kwamba Iran ilifanya uchunguzi mkali kuhusu utengenezaji wa zana za atomiki akisema mpango wa nchi yake wa nyuklia umekuwepo, upo na utaendelea kwa amani.

Katika ripoti iliyoshirikisha wanachama watano wa kudumu katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa China, Urusi, Marekani, Ufaransa, Uingereza pamoja na Ujerumani Balozi wa Uingereza John Sawers aliambia Baraza hilo kwamba nchi hizo zingependa mjumbe wa Umoja wa Ulaya anaeshughulikia maswala ya nchi za nje Javier Solana akutane na mwakilishi wa Iran katika maswala ya Nyuklia Saed Jalili ili wajaribu kuanzisha tena mazungumzo yatakayoleta suluhu katika swala hilo la nyuklia.

Bila kuelezea kwa undani Sawers alisema nchi hizo nne zilikuwa tayari kuongeza yale zilizoahidi Iran mwaka wa 2006 iwapo nchi hiyo ingesitisha mpango wake wa Nyuklia.

Siku moja baada ya Iran kuwekewa vikwazo vipya China kupitia kwa msemaji wake wa maswala ya nchi za nje imesema vikwazo hivyo havilengi kuiadhibu Iran ila kuweka diplomasia nzuri zaidi kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Hata hivyo msemaji huyo amesema vikwazo vipya ilivyowekewa Iran havitaathiri kivyovyote biashara kati ya nchi hizo mbili.

Japan kwa upande wake imepongeza hatua ya baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ikidai kwamba Iran imekuwa ikishirikiana na hasimu wake Korea Kaskazini.