1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yazidi kuzikosoa Nchi za Magharibi

P.Martin14 Machi 2008

Kufuatia kampeni ya juma moja,Wairani wenye haki ya kupiga kura leo wanawachagua wabunge wao huku serikali ya Iran ikizidi kuzikosoa nchi za Magharibi.

https://p.dw.com/p/DOH9
Iran's supreme leader Ayatollah Ali Khamenei casts his ballot in Iran's parliamentary elections in Tehran, Iran, Friday March 14, 2008.(AP Photo/Hasan Sarbakhshian)
Kiongozi wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamanei akipiga kura yake mjini Tehran,Ijumaa tarehe 14 mwezi Machi,2008.Picha: AP

Uchaguzi wa bunge unaofanywa nchini Iran hauhusiki kabisa na Marekani amesisitiza Rais wa Bunge Gholam Ali-Addad-Adel.Washington inajaribu kuleta mtengano wa taifa na kudhibiti bunge lakini haitofanikiwa.Kwani viongozi wengine wa kihafidhina wamechochea kampeni dhidi ya mbunge Noureddine Pir Mouazaem kwa sababu mwanasiasa huyo anaependelea mageuzi alikuwa na mahojiano kuhusu uchaguzi wa leo.

Lakini si Marekani tu iliyotuhumiwa kujaribu kuwasiliana na viongozi wenye siasa za wastani.Ujerumani nayo imetiwa katika kundi hilo.Kwani balozi wa Ujerumani Herbert Honsowitz mjini Tehran,amekosolewa vikali katika vyombo vya habari na taarifa za seraikali kuwa alikutana na kiongozi wa kundi la wapenda mageuzi,Mohamed-Reza Khatami na alisikiliza malalamiko ya mwanasiasa huyo.Lakini mwanadiplomasia Honsowitz anaeifahamu vizuri mno Iran na Mashariki ya Kati,hakushughulishwa na ukosoaji huo kwani yeye alikutana pia na wanasiasa wa kihafidhina.Hata hivyo Balozi Honsowitz amelaumiwa kuwa alikutana na Rais wa zamani wa Iran Mohammad Khatami na kuongezea kwamba mkutano huo ulikuwa siku moja kabla ya Umoja wa Mataifa hivi karibuni kuidhinisha vikwazo vipya dhidi ya Iran.

Ni dhahiri kuwa hiyo ilikuwa sehemu ya kampeni ya uchaguzi kwani tuhuma hizo ziliiibuka kabla ya uchaguzi.Juu ya hivyo tuhuma hizo haziwezi kupuuzwa na kuwekwa kando kwani zimegusa mada inayopandisha hisia za Wairani.Hakuna jambo linalochukiwa zaidi na kila Muirani kama vile wageni kuingilia mambo yao ya ndani. Mfano mmoja ni dai la Washington kutaka mabadiliko ya serikali pamoja na msimamo wake kuhusu mradi wa nyuklia wa Iran.

Lakini Iran imevunjwa moyo na hata kuhamakishwa na msimamo wa nchi za Ulaya na hasa ule wa Ujerumani kuhusu mgogoro wa nyuklia.Kwani kwa Wairani wengi Ujerumani ni rafiki wa kale na kwa sehemu kubwa hutazamwa kama ni mfano mzuri.Lakini siku za hivi karibuni mawazo hayo yamevurugika kwa sababu ya msimamo wa Berlin kuhusu mradi wa nyuklia wa Iran pamoja na suala la vikwazo.Iran imezoea hayo kutoka Marekani na siyo Ujerumani.

Hata hivyo,si Ujerumani tu bali nchi zote za Ulaya zijitayarishe kwa kipindi cha mvutano pamoja na Iran,kwani kisiasa nchi hizo zimeibwaga Iran kwa hivyo zitaadhibiwa na kuzidi kudharauliwa.Na ikumbukwe kuwa siasa zinapokwama,basi biashara pia hudorora.Hivi sasa tayari balozi wa Urusi anachukuliwa kama ni mwanadiplomasia muhimu kabisa wa kigeni mjini Tehran.Vile vile China,Japan na Korea ya Kusini ni washirika muhimu wa biashara wa Iran kuliko nchi zote za Umoja wa Ulaya.