1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq yaifungia Al-Jazeera, vituo vingine tisa

29 Aprili 2013

Seriakli ya Iraq imekifungia kituo cha televisheni cha kimataifa cha Aljazeera na vituo vingine tisa vya nchini humo siku ya Jumapili, baada ya kivituhumu kwa kuchochea vurugu za kidini.

https://p.dw.com/p/18OkK
Titel: "Logo Aljazeera" Die Genehmigung zur Veröffentlichung wurde eingeholt
Logo AljazeeraPicha: Aljazeera

Hatua hii imemulika wasiwasi unaozidi wa serikali inayoongozwa na washia, juu ya hali ya usalama inayozidi kudorora, wakati wa machafuko ya waumini wa kisunni na makabiliano yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 180 katika muda wa chini ya wiki moja. Kusimamishwa kwa vituo hivyo ambako utekelezaji wake ulianza mara moja kunaonekana kuvilenga hasa vituo vya kisunii vinavyojulikana kwa kuikosoa serikali ya waziri mkuu Nouri al-Malik.

Wanamgambo wenye silaha wanaoipinga serikali kutoka maeneo ya wasunni wakiandamana mjini Ramadi, mashariki mwa Baghdad.
Wanamgambo wenye silaha wanaoipinga serikali kutoka maeneo ya wasunni wakiandamana mjini Ramadi, mashariki mwa Baghdad.Picha: AFP/Getty Images

Pamoja na kituo cha Aljazeera, uamuzi huo uliviathiri vituo nane vya kisunni na kimoja cha kishia. hatua hii ya serikali imekuja huku utawala mjini Baghdad ukijaribu kukabiliana na ongezeko la machafuko nchini humo, yaliyoripuka siku chache zilizopita, baada ya vikosi vya usalama kuanzisha operesheni ya ukandamizaji dhidi ya kambi ya waandamanaji wa kisunni katika mji wa kati wa Hawija, na kuua watu 23, wakiwemo wanajeshi watatu.

Tangu wakati huo, zaidi ya watu 180 wameuawa katika mapigano na vikosi vya usalama na mashambulizi mengine. Wimbi la hivi karibuni la vurugu linafuatia miezi minne ya maandamano ya amani ya waislamu wa madhehebu ya sunni, dhidi ya serikali ya waziri mkuu Nouri al-Maliki. Watazamaji nchini Iraq watanedelea kutizama vituo hiyvo, lakini tangazo la kusitishwa kwake lililotolewa na tume ya mawasiliano na vyombo vya habari linasema kama vituo hivyo kumi vitajaribu kuendesha shughuli zake katika ardhi ya Iraq, vitakabiliwa na hatua za kisheria kutoka kwa vyombo vya usalama. Kimsingi amri hiyo inawazuia wanahabari kutoka vituo hivyo kufanya kazi zao nchini Iraq.

Aljazeera yashtushwa na kufungiwa

Mbunge wa Kisunni Dahfir al-Ani aliielezea hatua hiyo kama sehemu ya majaribio ya serikali kuficha umuagaji damu uliyofanyika mjini Hawija na kile kinachoendelea katika maeneo mengine nchini humo. Al-jazeera ilisema katika taarifa kuwa imeshangazwa na hatua hiyo ya serikali ya Iraq, na kuongeza kuwa imekuwa ikiripoti pande zote za habari nchini Iraq kwa miaka mingi. Aljazeera iliripoti kwa undani kuhusu mapinduzi katika mataifa ya kiarabu, na imekuwa ikiripoti kwa kiasi kikubwa kuhusu mgogoro unaondelea nchini Syria.

Magazeti na vyombo vingine vya habari vilianzishwa nchini Iraq baada ya kuanguka kwa utawala wa Saddam Hussein mwaka 2003, lakini nchi hiyo imeendelea kuwa mmoja yenye hatari zaidi kwa waandishi wa habari, ambapo zaidi ya 150 wameuawa tangu mwaka 1992, kwa mujibu wa kamati ya kulinda waandishi wa habari.

Waziri Mkuu wa Iraq Nouri al-Maliki.
Waziri Mkuu wa Iraq Nouri al-Maliki.Picha: AP

Iraq na serikali nyingine za mashariki ya kati ziliwahi kufunga ofisi za Al-Jazeera kwa muda huko nyuma, kwa sababu hazikupendezwa na jinsi inavyoripoti matukio. Vituo vingine tisa ambavyo leseni zake zimefungiwa na tume ya mawasiliano ya Iraq ni pamoja Al-Sharqiya na Al-Sharqiya News, ambacho kinaikosoa serikali mara kwa mara, na vituo vingine vidogo saba vikiwemo Salahuddin, Fallujah, Taghyeer, Baghdad, Babiliya, Anwar 2 na al-Gharbiya.

Televisheni ya Baghdad yasema ni uamuzi wa kisiasa

Televisheni ya Baghdad iliyopo mjini Baghdad, ilisema uamuzi huo ulikuwa ni wa kisisiasa. "Serikali ya Iraq haina uvumilivu kwa maoni yanayokinzana na wanajaribu kunyamanzisha sauti zinazokwenda kinyume na msismamo rasmi," alisema Omar Subhi, mkurugenzi wa kitengo cha habari. Alisema Televisheni hiyo ilikuwa na wasiwasi juu ya usalama wa wafanyakazi wake, ikihofia kuwa vikosi vya usalama vinaweza kuwafukuza.

Katika taarifa iliyochapishwa katika mtandao wake, tume ya habari ya serikali ilivilaumu vituo vilivyofungiwa kwa kuongezeka kwa wasiwasi wa kidini, ambao unachochea vurugu zilizofuatia mapigano ya maafa mjini Hawija. Tume hiyo ilivishtumu vituo kwa kutoa ripoti za upotoshaji na zilizotiwa chumvi, kutangaza wito wa dhahiri wa uvunjivu wa amani, na kuanzisha mashambulizi ya kihalifu ya kulipiza kisasi dhidi ya vyombo vya usalama. Pia ilivilaumu vyombo hivyo kuyatangaza makundi ya kigaidi yaliyopigwa marufuku, yaliyotenda uhalifu dhidi ya watu wa Iraq.

Osama Abdul-Rahman, mfanyakazi wa serikali wa madhehebu ya kisunni kutoka kaskazini mwa Baghdad, alisema serikali inatumia sera ya ndumila kuwili kuhusiana na vyombo vya habari, kwa kuvifumbia macho vituo kadhaa vya kishia ambavyo anadai vinachochea vurugu. "Vituo vilivyo karibu na vyama vikuu vya kishia na hata televisheni ya taifa pia vinarusha vipindi vya ubaguzi wa kidini vinavyochochea vurugu muda wote, lakini hakuna mtu anaevisimamisha," aliongeza.

Wananchi wakibeba jeneza la mwanajeshi alieuwawa katika vurugu za hivi karibuni.
Wananchi wakibeba jeneza la mwanajeshi alieuwawa katika vurugu za hivi karibuni.Picha: Reuters

HRW yasema madai ya serikali yana mashaka

Erin Evers, mtafiti wa masuala ya mashariki ya kati kutoka shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch, aliyaita madai ya serikali kwamba imevivhukuliwa hatua vituo vya televisheni kwa kuchochea ubaguzi wa kidini kuwa ya mashaka, kwa kuzingatia "historia yake endelevu ya ukandamizaji dhidi ya vyombo vya habari - hasa vyombo vya habari vinavyoegemea upinzani -hasa katika nyakati nyeti kisiasa."

"Kufungiwa kwa vituo hivyo ni ushahidi mwingine kuwa serikali inataka kuzuia kuripotiwa kwa habari wasizozipenda," alisema Evers. Aliituhumu tume ya habari ya Iraq kwa kuchanganya ripoti ya hotuba iliyo na vidokezo vya ubaguzi wa kidini na kuchochea kwa wazi kwa vurugu za kidini. "Haya ni mambo mawili tofauti kabisaa na lwa kwanza linalindwa chini ya sheria za kimataifa na za Iraq pia," alisema.

Uamuzi wa kufungia vituo hivyo ulikuwa wakati ambapo al-Maliki akihudhuria isivyo kawaida katika maziko rasmi ya wanajeshi watano waliouawa siku ya Jumamosi, na watu wenye silaha katika mkoa wa wasunni wa Anbar. Polisi katika mkoa huo ilisema wanajeshi hao waliuawa katika mapigano baada ya gari lao kusimamishwa karibu na kambi ya maandamano ya wasunni.

Matukio ya mashambulizi kama hili yameongezeka nchini Iraq.
Matukio ya mashambulizi kama hili yameongezeka nchini Iraq.Picha: picture-alliance/dpa

Serikali ilitoa muda wa masaa 24 kwa waandaji wa maandamano hayo kukabidhi watu waliohusika na mauaji hayo, au wakabiliwe na hatua kali. Lakini hakuna mtu aliekabidhiwa na muda uliyotolewa umepita. Siku ya Jumamosi, watu wenye silaha wakitumia bunduki zilizofungiwa vifaa vya kuzuia sauti, walipiga risasi na kuwauwa viongozi wawili wa kikabila wasunni katika matukio mawili tofauti ya kusini mwa Baghdad.

Miripuko yazidi kutikisa

Wakati huo huo, miripuko mitatu ya mabomu yaliyotegwa kwenye magari imesababisha vifo vya watu wasiopungua 20 kusini mwa Iraq siku ya Jumatatu, katika maeneo yanayokaliwa na washia wengi. Mripuko moja ulitokea karibu na soko, wakati mwingine ulitokea karibu na mkusanyiko wa wafanyakazi katika mji wa Amara, uliyopo kilomita 400 kusini-mashariki mwa Baghdad. Mripuko huo uliua watu 16 na kujeruhi 25.

Kkatika mji wa Diwaniya, uliyoko kilomita 150 kusini-magharibi mwa Baghdad, bomu la kwenye gari liliripuka karibu na mgahawa, na kuua watu wanne na kujeruhi wengine 11. Kuongezeka kwa vurugu hizi kunaongeza hofu ya kurudisha vurugu za kidini zilizoipeleka nchi hiyo karibu na kuripuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 2006 na 2007.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape
Mhariri: Daniel Gakuba