1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IS inajihami kijeshi katika maeneo ya mizozo

Bruce Amani
7 Februari 2017

Kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu – IS linajihami kijeshi nchini Afghanistan, Iraq, Libya na Syria lakini kwa sehemu likibadili mkakati na kuhamia katika mbinu ya kuwa na mawasiliano ya siri

https://p.dw.com/p/2X7g1
Irak Kampf um Mosul
Picha: Getty Images/AFP/A. Al-Rubaye

Katika ripoti yake mpya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kitisho cha mashambulizi katika viwanja vya ndege na ndege kinabakia kuwa kikubwa. Kundi la IS linaendelea kuwahimiza wafuasi wake nje ya maeneo ya migogoro kufanya mashambulizi wakitumia mahusiano ya makundi yaliyopo ndani ya nchi hizo.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, inasema nchi wanachama zilionyesha kuwa mawasiliano ya ndani na usajili wa wapiganaji wa IS unahamia sana katika upande wa mbinu za kisiri, kama vile lugha ya siri ya mtandao wa intaneti na usimbaji fiche.

Hatahivyo, Guterres amesema kampeni za kijeshi dhidi ya IS zinakuwa na mafanikio makubwa. Amesema kundi hilo limepoteza idadi kubwa ya wapiganaji wake pamoja na maeneo wanayodhibiti ambapo pamoja na kudorora hali ya kifedha ya kundi hilo wamepunguza kwa kiasi kikubwa usajili wake wa wapiganaji wa kigeni.

New York UN Generalsekretär Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Reuters/S. Keith

Serikali mbalimbali za nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimeongeza udhibiti wa mipaka yake na hivyo kupunguza mmiminiko wa wapiganaji wa kigeni kuelekea Iraq na Syria. Kwa upande wa kifedha, kundi hilo linaendesha harakati zake kwa bajeti ya "dharura”, lakini mapato yake yanabakia kuwa yale yale – mafuta na gesi, na kuwatoza wananchi kodi ambayo kwa pamoja yanajumuisha asilimia 80 ya mapato yake. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq unakadiria kuwa IS ilipata karibu dola milioni 260 kutokana na mauzo ya mafuta mwaka jana, hasa kutoka kwa visima vya mafuta katika mkoa wa Deir el-Zour nchini Syria. Guterres anasema hiyo ni karibu nusu ya makadirio ya mwaka wa 2015 ya karibu dola milioni 500.

Akigusia Ulaya, Guterres amesema nchi wanachama kwa sasa zinakadiria kuwa "kitisho cha kutokea mashambulizi makubwa bado kipo”. Nchi moja ambayo haijatajwa ilisema kuwa sio wapiganaji wote wa IS waliotumwa Ulaya kufanya mashambulizi ya mwaka jana mjini Paris na Brussels walitambuliwa na kukamatwa.

Türkei Razzien gegen mutmaßliche IS-Kämpfer
Kikosi cha kupambana na ugaidi nchini UturukiPicha: picture-alliance/AP Photo

Nchini Libya, Guterres amesema operesheni ya kijeshi iliifurusha IS kutoka mjini Sirte, mojawapo ya ngome zake muhimu nje ya Iraq na Syria, ambayo ilipunguza raslimali za kundi hilo.

Lakini wapiganaji wa IS wamehamia maeneo mengine ya Libya, na idadi yao inakadiriwa na nchi wanachama kuwa kati ya mamia kadhaa hadi 3,000.

Guterres amesema IS pia imeimarisha uwapo wake Afrika Magharibi na kusini mwa jangwa la sahara, akitaja mashambulizi ya karibuni nchini Nigeria na Burkina Faso yaliyohusishwana kundi hilo la kigaidi. Baraza la Usalama Desemba mwaka jana lilitoa wito kwa nchi zote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa kuzingatia kuweka sheria na mifumo ya kushughulikia ukubwa wa kitisho cha IS na kushirikiana katika kubadilishana taarifa za kijasusi, maelezo muhimu ya watu na ya kifedha.

Guterres, mkuu wa zamani wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi, pia amesisitiza kuwa wakimbizi wengi, barani Ulaya na kwengineko ulimwenguni, hawana mahusiano na ugaidi na wamekimbia mataifa yao ya uzawa ili kuepuka mateso na vita .

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman