1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISLAMABAD: Bhutto azuru mji wa Lahore

11 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CBJy

Kiongozi wa upinzani nchini Pakistan, Benazir Bhutto, leo anazuru mji wa Lahore mashariki mwa Pakistan.

Katika ziara yake hiyo, Bi Bhutto yuko katika awamu mpya ya kampeni yake kujaribu kurejesha demokrasia nchini Paksitan.

Waziri mkuu huyo wa zamani wa Pakistan ameileza nchi hyio kuwa jiko la gesi ambalo linasubiri kulipuka wakati wowote akizingatia vurugu zinazoendelea nchini Pakistan kwa wakati huu.

Hapo awali alishiriki kwenye maandamano ya wanachama wa vyombo vya habari mjini Islamabad waliopinga ukandamizaji wa uhuru katika kupata habari.

Kwa kutangaza hali ya hatari nchini Pakistan, rais Pervez Musharaf amesimamisha utekelezwaji wa katiba na kuwaondoa majaji wa mahakama kuu.

Jenerali Musharaf anatarajiwa hii leo kufanya mkutano wa kwanza na waandishi wa habari tangu alipotangaza hali ya hatari, ambapo huenda akazungumzia hatima ya katiba ya Pakistan, kuzuiliwa waandishi wa habari kufanya kazi na kutangaza tarehe ya uchaguzi wa bunge.