1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Islamabad. Polisi wavunja maandamano.

7 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/C799

Polisi wa Pakistan wametumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi na virungu kuvunja maandamano ya mamia ya waungaji mkono wa waziri mkuu wa zamani Benazir Bhutto ambao walikuwa wakiandamana kuelekea katika bunge mjini Islamabad . Polisi waliingia dakika chache baada ya waziri mkuu wa zamani kutoa wito wa kufanyika maandamano yatakayofanyika siku ya Ijumaa. Wanaharakati watatu wamekamatwa. Bhutto amesema waungaji mkono wa upinzani watafanya maandamano siku ya Ijumaa mjini rawalpindi na ametoa wito tena kwa jenerali Musharraf kujiuzulu.

Wakati huo huo wito wa Benazir Bhutto kuwataka watu kutotii hali ya hatari iliyotangazwa na rais Musharraf inaonekana na wapinzani wake na wachunguzi wa mambo kuwa anataka kupata makubaliano ya kugawana madaraka. Shaka imezidi kutokana na kuungwa kwake mkono na Marekani na Uingereza katika majadiliano yake ya kugawana madaraka na Musharraf, mshirika wao mkuu kuhusu mapambano dhidi ya ugaidi.Afisa mmoja wa serikali amewaambia waandishi wa habari kuwa amri ya hali ya hatari inaweza kuondolewa katika muda wa wiki mbili ama tatu zijazo.