1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISLAMABAD : Serikali ya mpito yaandaliwa

15 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CG1A

Rais Pervez Musharraf na wasaidizi wake wamekuwa wakikamilisha uundaji wa serikali ya mpito leo hii wakati wapinzani wake wawili wakuu wakianza mazungumzo ya kuunda muungano dhidi yake.

Leo ni siku ya mwisho wa muda wa kipindi cha bunge la sasa wa miaka mitano na muhula wa Musharraf wa kuwa rais wa Pakistan pia unamalizika leo hii juu ya kwamba ameuongeza kwa kutangaza utawala wa hali ya hatari.

Serikali hiyo ya muda itakuwa na majukumu ya kuingoza Pakistan kwenye uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika tarehe 9 mwezi wa Januari.

Wakati huo huo Mawaziri Wakuu wa zamani wa Pakistan Benazir Bhutto na Nawaz Sharrif wamekubaliana kuungana dhidi ya Rais Musharraf.

Viongozi hao wawili wa upinzani wamezungumza kwa njia ya simu hapo jana na wako tayari kusahao tofauti zao kwa ajili ya kuendesha mapambano ya pamoja kumn’gowa Musharraf ambaye anashikilia wadhifa wa urais na ukuu wa majeshi.

Bhutto hivi sasa amezuiliwa nyumbani katika mji wa Lahore wakati Sharif yuko uhamishoni nchini Saudi Arabia.

Naye mpinzani mwengine wa Pakistan mchezaji wa kriketi mashuhuri wa zamani Imran Khan amefunguliwa mashtaka ya uhaini ya kuvuruga amani kwa kuhuhudhuria maandamano ya wanafunzi dhidi ya Musharraf.