1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISLAMABAD: Steinmeier ziarani Pakistan

23 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBzF

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, yumo nchini Pakistan kwa ziara rasmi. Lengo la ziara yake hiyo ni kufanya mazungumzo kuhusu machafuko yanayoendelea katika nchi jirani ya Afghanistan na uhusiano unaolegalega baina ya serikali ya mjini Islamabad na Kabul.

Waziri Steinmeier aliyeitembelea Afghanistan hapo jana, anatarajiwa kukutana hii leo na waziri mkuu wa Pakistan, Shaukat Aziz na waziri wa mashauri ya kigeni, Khurshid Kasuri, mjini Islamabad.

Ziara ya Frank Walter Steinmeier, ni sehemu ya mpango wa Ujerumani kupitia mataifa yaliyoendelea zaidi kiviwanda dunia ya G8, kutaka kuboresha mahusiano baina ya serikali za Afghanistan na Pakistan.

Nchi hizo mbili ni washirika wa Marekani katika vita dhidi ya ugaidi wa kimataifa lakini uhusiano kati yao unaelezwa kuwa mbaya zaidi tangu waasi wa kundi la Taliban walipong ´olewa madarakani mnamo mwaka wa 2001.

Wajumbe wa Pakistan na Afghanistan wanatarajiwa kuhudhiria mkutano wa mawaziri wa mashauri ya kigeni wa nchi za G8 mjini Potsdam hapa Ujerumani wiki ijayo.