1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Islamabad. Viongozi kadha wakamatwa.

4 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/C79x

Maafisa wa Pakistan wamewakamata wanaharakati viongozi wa upinzani katika msako ulioanzishwa saa chache baada ya rais Pervez Musharraf kutangaza amri ya hali ya hatari nchini humo.

Polisi wamewakamata kiasi cha wanaharakati 300 wanaopigania haki, wanasheria na wafanyakazi wa upinzani, ikiwa ni pamoja na kiongozi mkuu wa chama kinachoongozwa na waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif . Hapo mapema jenerali Musharraf , alitetea amri hiyo ya hali ya hatari, akisema kuwa amechukua hatua hiyo kupambana na hali inayozidi kukua ya ghasia na wabunge ambao wanajaribu kuidhoofisha nchi hiyo.

Akizungumzia kuhusu hatua hiyo waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Benazir Bhuto amesema kuwa ana shaka na hatua aliyoichukua Musharraf.

Wakati amri ya hali ya hatari ikiwekwa , jaji mkuu nchini humo ameondolewa na mahakama kuu kuzingirwa na vikosi vya jeshi. Mahakama ilikuwa iamue iwapo Musharraf alistahili kugombea kiti cha urais mwezi uliopita wakati akiwa mkuu wa majeshi.

Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Benazir Bhutto , ambaye amerejea hivi karibuni nchini humo baada ya miaka nane ya kuishi uhamishoni , ameahidi kuchukua hatua dhidi ya amri hiyo ambayo ameeita sheria ya kijeshi. Kiongozi mwingine wa chama cha upinzani Amran Khan amefanikiwa kutoroka kutoka kizuizi cha nyumbani kwake. Waziri mkuu Shaukat Aziz amesema kuwa amri hiyo itabakia hadi pale itakapoamuliwa vingine.