1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISLAMABAD: Waziri ajiuzulu kupinga rais Musharaf kutaka kubakia madarakani

28 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBV9

Waziri anayehusika na teknolojia ya habari nchini Pakistan, Ishaq Khan Khakwani, amejiuzulu kupinga mpango wa rais Pervez Musharaf kutaka kuendelea kubakia madarakani.

Waziri huyo pia ametaka kufanyike mdahalo wa kitaifa utakaovijumulisha vyama vya kisiasa vya upinzani.

Wakati huo huo, waziri mkuu wa Pakistan, Shaukat Aziz, ametoa mwito kufanyike mdahalo wa kisiasa nchini humo huku rais Pervez Musharaf akijiandaa kutafuta kuchaguliwa tena kuwa rais wa Pakistan.

Hata hivyo Shaukat Aziz amesema serikali haina mpango wa kubatilisha uamuzi wa kuwapiga marufuku viongozi wa upinzani walio uhamishoni kuchukua tena wadhifa wa waziri mkuu.

Jenerali Musharaf, mshirika muhimu wa Marekani aliyenyakua madaraka katika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka wa 1999, ana mpango wa kuwaomba wabunge mwezi ujao au mwezi Oktoba mwaka huu, wampe awamu nyengine ya miaka mitano aendelee kuwa rais.

Lakini nafasi yake ya kuendelea kubakia madarakani imepungua huku utawala wa kijeshi ukikaribia kumalizika nchini Pakistan na mawaziri wakuu wa zamani, Benazir Bhutto, na Nawaz Sharif, wakipanga kurejea nchini humo.