1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISRAEL YASEMA ITAENDELEA KUISHAMBULIA GAZA

Liongo, Aboubakary Jumaa28 Februari 2008
https://p.dw.com/p/DF2i
Waziri Mkuu wa Israel Ehud OlmertPicha: AP


Majeshi ya Israel yamekuwa katika harakati kubwa za kushambulia Gaza ambapo hapo jana wanamgambo sita wa Hamas waliuawa kutokana na mashambulizi hayo ya Israel.


Kauli hiyo ya Waziri Mkuu wa Israel inakuja huku Marekani ikielezea wasi wasi wake juu hali ya maisha ya wapalestina huko Gaza.


Waziri Mkuu huyo wa Israel ambaye yuko katika ziara ya nchini Japan aliwaambia waandishi wa habari ya kwamba Israel haotositisha mashambulizi hayo.


Olmet amesema kuwa amemuelezea Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleza Rice ya kwamba Israel itaendelea na mashambulizi yake kuhakikisha kuwa  magaidi wanapata kipigo kikali.


Condoleza Rice ambaye naye yuko katika ziara nchini Japan ametangaza kuwa atakwenda katika eneo la mashariki ya kati wiki ijayo ili kujaribu kuyapa nguvu mazungumzo ya mpango wa amani katika eneo hilo yanaonekana kukwama.


Wanamgambo wa Hamas hapo jana walivurumisha makombora katika eneo la kusini mwa Israel ambapo muisrael mmoja katika chuo kikuu  nje kidogo ya mji wa Sdetot aliuawa.


Hicho ni kifo cha kwanza kwa Muisrael toka kundi la Hamas lilipochukua udhibiti wa eneo la Gaza mwezi Juni mwaka jana, na kundi hilo limesema hatua hiyo kulipiza kisasi kutokana na kuawa kwa wapiganaji wake.


Waziri Mkuu Olmet akizungzmzia juu ya shambulizi hilo alisema kuwa kwa sasa wako katika kilele cha mapambano na kwamba wataendelea na mapambano hayo mpaka vitisho vya Hamas vitakapokoma.


Na katika kuthibitisha kauli hiyo, Israel ilifanya mashambulizi makali huko Gaza ambapo mbali ya wanamgambo sita wa Hamas  wapalestina watano waliuawa akiwemo mtoto wa mwanasheria mashuhuri wa Hamas Hamza al-Haya, kama alivyothibitisha daktari huyu wa kipalestina aliyekataa kutaja jina lake alipozungumza na deutche welle.


Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani Condoleza Rice akizungumzia hali hiyo alisema kuwa  changamoto kubwa iliyopo ni kuwa na mtizamo wa kuwepo kwa taifa la Palestina moja lenye mshikamano.


Marekani na mataifa mengine ya magharibi pamoja na Israel zinamuunga mkono Rais wa mamlaka ya Palestina kutoka chama cha Fatah Mahamoud Abbas anayedhibiti eneo la ukingo wa Magharibi.


Mahamoud Abbas alishutumu mashambulizi la Hamas hapo jana dhidi ya Israel yaliyosababisha kifo cha mtu mmoja, mashambulizi ambayo yameamsha zaidi hasira za Israel.


Hata hivyo Hamas imemlaumu Abbas ikisema kuwa kauli yake hiyo inawapa kiburi Israel cha kuendelea na uvamizi wake huko Gaza.


Takriban watu 219 wengi wakiwa ni wanamgambo wa Hamas wamekwishauawa mpaka sasa toka mazungumzo ya amani yalipofufuliwa huko mashariki ya kati.


Lakini mapigano ya hivi karibuni yamezidi kuhatarisha mafanikio ya mazungumzo hayo ya amani yanayofadhiliwa na Marekani, ambapo Rais George Bush ana matumaini ya kuona mafanikio yanapatikana kabla ya kipindi chake cha kukaa madarakani hakijamalizika mwakani.