1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na Hamas zalaumiwa

Abdul Mtullya/ZPR24 Februari 2009

Shirika linalotetea haki za binadamu duniani Amnesty International limezilaumu Israel na Hamas kwa kutenda uhalifu wa kivita wakati wa vita kwenye Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/H0Bg
Wanajeshi wa Israel wakiingia GazaPicha: AP

Shirika hilo limesema katika ripoti yake kuwa lina ushahidi unaothibitisha kuwa pande zote mbili ziliwashambulia raia kwa silaha kutoka nje.


Katika ripoti yake shirika la Amnesty International limezilaumu Israel na Hamas kwa kutenda uhalifu wa kivita na limeutaka Umoja wa mataifa uweke vikwazo vya silaha dhidi ya Israel na Hamas.

Israel inalaumiwa kwa kutumia mabomu ya phosphorous nyeupe, silaha zinazokatazwa chini ya sheria la kimataifa.

Shirika la Amnesty International pia limeilamu Hamas kwa kufanya mashambulio holela ya roketi dhidi ya raia kusini mwa Israel.

Kutokana na hayo jumuiya hiyo ya kutetea haki za binadamu inataka pande mbili hizo ziwekewe vikwazo vya silaha.

Lakini Israel na Hamas zimesema kuwa uchunguzi uliofanywa na shirika la Amnesty International una makosa kama alivyosisitiza msemaji wa serikali ya Israeal Mark Regev.


´´Ripoti ya shirika la Amnesty International kimsingi ina makosa na taratibu zilizotumika ni za utatanishi.

Kwanza kabisa ripoti hiyo inarejelea habari zilizotolewa na Hamas. Habari hizo ni tatanishi.Watu wengi wana mashaka juu ya ukweli wa habari hizo.Jambo la pili ni kwamba taarifa ya Amnesty International imepuuza hali tata za mapambano.

Palikuwa na mapigano, na Hamas iliwatumia raia kikatili kwa kuwageuza ngao´´


Lakini shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limekanusha madai ya Israel.

Aliyeongoza uchunguzi kwa niaba ya shirika hilo Donatella Rovera amesema kuwa shirika lake halikutumia habari kutoka kwa Hamas.

Amesema madai hayo ni kichekesho.Ameeleza kuwa taarifa ya shirika hilo imejaa hoja za kweli,picha na takwimu.

Amesema wachunguzi waligundua mabaki mengi ya roketi na magurunedi ya Israel,shuleni,kwenye hospitali na katika nyumba za watu.Bibi Donatella Rovera amesema raia wa kipalestina walitumiwa kama ngao, lakini siyo na Hamas bali na majeshi ya israel.


´´Askari wa Israel waliwatisha kwa silaha raia wa kipalestina na kuwalazimisha kuingia katika nyumba na kutafuta mitego ya mabomu. Pia waliwalazimisha kungia katika nyumba palipokuwapo wapiganaji wa kipalestina au katika nyumba zilizotumiwa kama ngome na askari wa Israel.

Hatukuona ishara ya matendo kama hayo kutoka kwa wapalestina"


Juu ya uhalifu wa Hamas na makundi mengine ya wapiganaji wa kipalestina shirika la hilo la Amnesty International limesema, uhalifu huo umetokana na mashambulio ya roketi katika sehemu za Isreal.Shirika hilo imesema hayo siyo tu kwamba hayakubaliki bali pia ni uhalifu wa kivita na kwamba Hamas inapaswa kukiri hayo.

Hatahivyo Hamas kwa upande wake imesema kuwa uchunguzi wa Shirika hilo haukuwa na mizani sawa, haukuwa wa haki na umewaweka wahanga na wahalifu katika safu moja.