1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na Marekani

24 Machi 2010

Netanyahu akutana na Obama mjini Washington.

https://p.dw.com/p/MagS
Waziri-mkuu NetanyahuPicha: AP

Rais Barack Obama wa Marekani na waziri-mkuu Benjamin Netanyahu wa Israel , walikutana jana faraghani mjini Washington, kwa muda wa saa 1 na nusu wakijaribu kupunguza mvutano wao unaoathiri usuhuba kati ya washirika hawa 2 wa chanda na pete. Mazungumzo ya jana hayaoneshi kuzaa matunda mema katika juhudi za kuhimiza usoni utaratibu wa amani wa Mashariki ya kati.

Mkutano wao kinyume na desturi, ulikuwa wa hadhi ya nchini kwa mgeni mashuhuri kama waziri-mkuu wa dola la Israel na ambao ulifanyika baada ya waziri-mkuu Netanyahu kutamba hadharani akibisha wale wanaokosoa sera zake za ujenzi wa maskani zaidi katika ardhi za wapalestina huko Jeruselem ya Mashariki na ukingo wa Magharibi.

Afisi ya waziri-mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, imearifu kwamba mkutano wa viongozi hao 2 ulifanyika katika hali njema na kuongeza kuwa washauri wa pande zote mbili waliendelea na kikao kilichotazamiwa kudumu siku nzima.

Taarifa ya Israel , haikutaja mengi zaidi jinsi mazungumzo yalivyo kwenda kati ya Obama na Netanyahu,lakini, wachunguzi wanahisi kubakia kwa Bw.Netanyahu kwa masaa 2 zaidi huko ikulu kwa mazungumzo , ni ishara mambo yalikuwa magumu .

Maafisa wa Ikulu ya Marekani, walikataa kusema hali hasa ilivyokuwa wakati wa mazungumzo ya rais Obama na Netanyahu na wala hawakusema iwapo maafikiano yalifikiwa kwenye mazungumzo hayo.

Mzozo mkubwa wa kidiplomasia, uliibuka kati ya washirika hawa 2 wa chanda na pete mapema mwezi huu pale Israel, ilipotangaza mipango ya ujenzi wa maskani 1.600 ya wayahudi katika eneo la waarabu la Mashariki mwa Jeruselem wakati wa ziara ya makamo-rais wa Marekani, Joe Biden, nchini Israel.

Tangazo hilo lilitokea siku 2 tu baada ya wapalestina kuridhia shingo upande mazungumzo yasio moja kwa moja na Israel na likawa pigo kali kwa juhudi za Marekani za miezi kadhaa za kuyafufua mazungumzo ya amani ya mgogoro wa Mashariki ya Kati.

Baada ya matamshi makali ya makamo-rais Joe Biden, huko Jeruselem, waziri wa nje wa Marekani, bibi Hillary Clinton, aliikosoa Israel kwa tangazo lake la ujnezi wa maskani:

"Ujenzi mpya wa maskani Mashariki mwa Jeruselem na ukingo wa Magharibi, unaharibu imani kwa pande zote mbili na unahatarisha mazungumzo yasio ya moja kwa moja ambayo ni hatua ya kwanza kuelekea mazungumzo kamili ambayo pande zote mbili zinadai zinayataka na zinayahitaji."

Nae Bw.Khatib, mjumbe wa Mmalaka ya Ndani ya Wapalestina , akijibu matamashi ya ukaidi aliotoa waziri-mkuu Netanyahu huko Washington, kuhusu ujenzi wa maskani kuwa, wayahudi wakijenga Jeruselem tangu miaka 3000 iliopita na kuwa wanacho jenga Jeruselem sio maskani, bali mji wao mkuu, alijibu:

"Matamshi ya hivi punde ya waziri-mkuu Netanyahu yanaendeleza ujenzi usio-halali mashariki mwa Jeruselem na yanavunja moyo."

Israel, iliinyakua sehemu ya waarabu ya Mashariki ya Jeruselem, katika vita vya Juni,1967 pamoja na Ukingo mzima wa magharibi na inaufikiria mji mzima wa Jeruselem ni mali yake.Wapalestina lakini, wanapanga sehemu yao ya mashariki ya jiji hilo la Jeruselem kuwa ndio mji mkuu wa dola lao kuu.

Wakati wa ziara ya siku 3 ya waziri mkuu Netanyahu mjini Washington,akishinikizwa na washirika wake wa mrengo wa kulia katika serikali ya muungano ya Israel, hakuonesha nia ya kuregeza kamba juu ya ujenzi wa maskani alao kabla ya kikao cha jana na rais Obama.

Wachunguzi wanahisi, ikiwa Netanyahu alihisi Obama ni rais dhaifu wakati huu ,basi alikosea.Kwani, baada ya ushindi wake jana wa kupitisha mageuzi ya bima ya afya, Obama, amebainisha nguvu zake na sasa anatazamiwa kwa ari na kasi mpya, kulikabili tatizo la Mashariki ya kati kama alivyouahidi ulimwengu wa kiarabu na wa kiislamu katika hotuba yake mwaka jana mjini Cairo.

Kabla ya kuonana na Obama, Netanyahu, aliwaambia wabunge wa Marekani kuwa anahofia mazungumzo ya amani yaliosimama tangu Desemba 2008,yamkini, yakachelewesha kwa mwaka mmoja, isipokuwa wapalestina wanaachana na sharti lao kuwa kwanza ujnezi wa maskani usimamishwe kamili.

Mwandishi: Ramadhan Ali/RTRE

Uhariri: M-Abdulrahman