1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na Palestina zashindwa kuafikiana

26 Machi 2010

Israel na Marekani zimeshindwa kufikia makubaliano kuhusu suala la kuyaongeza makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo la Jerusalem Mashariki.

https://p.dw.com/p/Mct0
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: AP

Kwa upande wake Israel inashikilia kuwa kamwe haitaibadili sera yake kuhusu suala hilo nayo Marekani inaishikiza iusimamishe kabisa ujenzi huo.

Wakati huohuo kulingana na kura ya maoni,asilimia 48 ya Waisraeli wanaamini kuwa Rais Obama anawaunga waPalestina.

Yote hayo yametokea siku moja baada ya Waziri Mkuu Netanyahu kuikamilisha ziara yake ya Washington.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotokea kwenye afisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu,sera ya Israel kuhusu ujenzi katika eneo la Jerusalem Mashariki katu haitobadilika.

Taarifa hiyo inaendelea kueleza kuwa uongozi wote wa Israel umekuwa ukilitimiza hilo kwa kipindi cha miaka 42 iliyopita.Kauli hizo zimetolewa baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuerejea nyumbani siku moja baada ya kufanya ziara Marekani ambayo inaonekana kuwa haikuleta tija yoyote ukiuzingatia mvutano huo.

Marekani inaripotiwa kuwa inaishinikiza Israel kuchukua hatua kadhaa zitakazoyawezesha mazungumzo ya kutafuta amani ya kudumu katika eneo la Mashariki ya Kati yanaanzishwa tena kati yao na Palestina.

Ujenzi mpya wa makazi katika eneo la Jerusalem Mashariki unapunguza kuaminiana kati ya pande zote mbili na unazitia hatarini harakati za kuyaanzisha tenamazungumzo ya kutafuta amani ambayo ni hatua ya kwanza ya majadiliano kamili ambayo wahusika wote wanahitaji.

Kwa sasa Israel bado haijatoa tamko rasmi kuhusu shinikizo hizo za Marekani.

Wakati huohuo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anajiandaa kukutana na baraza la mawaziri ili kulijadili suala hilo baadaye hii leo.

Hata hivyo duru za vyombo vya habari vyaIsrael zinaeleza kuwa makubaliano ya haraka huenda yasifikiwe kama inavyotarajiwa.Kulingana na Katibu wa Baraza la mawaziri,Zvi Hauser,kikao hicho kitalijadili suala hilo kwa kina na Israel itautangaza msimamo wake kwa kuzingatia maslahi yao.

Mbali ya suala la kusitisha ujenzi wa makazi ya walowezi, Marekani inaripotiwa kuwa inaitaka Israel pia kuwaachia huru mamia ya wafunga wa Kipalestina inaowazuwia.

Ziara hiyo ya Netanyahu kamwe haikupewa uzito katika vyombo vya habari na wala kiongozi huyo hakupata fursa ya kufanya mkutano na waandishi wa habari.

Mvutano wa aina hii wa kidiplomasia kati ya Marekani na mwandani wake Israel haujawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miongo mingi iliyopita.

Hata hivyo msemaji wa serikali ya Israel Nir Hefetz anashikilia kuwa nchi yao na Marekani ziko karibu kufikia makubaliano.

Kwa upande wake msemajai wa serikali ya Mamlaka ya Palestina Khatib Ghassan alisema

´´Kauli za hivi karibuni za Netanyahu kuhusu ujenzi haramu wa makazi katika eneo la Jerusalem Mashariki zinavunja moyo kwani ni sawa na kuzipuuza juhudi za Marekani na jamii ya kimataifa´´.

Kwa upande mwengine Wayahudi wengi wanaamini kuwa Rais Obama anaiunga mkono Palestina katika mvutano huu.

Kulingana na kura ya maoni iliyochapishwa katika gazeti la Jerusalem Post la leo,asilimia 48 ya Waisraeli wanaamini Rais Obama anaiunga mkono Palestina na asilimia 9 ndio wanaoonakuwa anawaunga mkono.

Kura hiyo ya maoni ilifanyika mwanzoni mwa wili hii baada ya mvutano kati ya Rais Obama na Israel kuongezeka katika kipindi cha wiki chache zilizopita.

Mvutano huo wa kidiplomasia ulianza baada ya serikali ya Israel kutangaza kuwa ina mpango wa kujenga makazi 1600 ya ziada ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo la Jerusalem Mashariki.

Kulingana na mtazamo wa Wapalestina,Jerusalem ndio utakaokuwa mji mkuu wa taifa lao waliloahidiwa.Kwa sasa Wapalestina wamekataa katakata kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Israel mpaka ujenzi huo usimamishwe kabisa.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya-AFPE/DPAE

Mhariri Aboubakary Liongo