1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaanza operesheni ya ardhini Gaza

18 Julai 2014

Vikosi vya Israel vikisaidiwa na vifaru na ndege za kivita vimeingia kwenye kingo za Ukanda wa Gaza katika operesheni kubwa ya kuangamiza mahandaki ya Hamas ambayo kundi hilo limesema itashindwa.

https://p.dw.com/p/1Ceyj
Vifaru vya Israel vikielekea kwenye mpaka wa Gaza.
Vifaru vya Israel vikielekea kwenye mpaka wa Gaza.Picha: picture-alliance/dpa

Wakati mashambulizi hayo ya Israel kwa Gaza yakiingia siku yake ya 11 kwa jeshi la nchi hiyo kuushambulia ukanda huo wa mwambao kwa njia ya anga na majini halikadhalika kwa kutumia vifaru viliyokusanywa mpakani, idadi ya maafa ya Wapalestina imeongezeka na kupindukia 260.

Raia wamekuwa wakikimbia maeneo yenye kupakana na mpaka wa Israel ambapo zaidi ya watu 30,000 wametafuta higadhi kwenye vituo vya Umoja wa Mataifa. Miongoni mwa waliouwawa wakati wa mashambulizi hayo ya usiku ni mwanajeshi mmoja wa Israel na mtoto mchanga wa miezi sita.

Taifa hilo la Kiyahudi limesema linaendelea na operesheni kuangamiza mitandao ya mahandaki iliyojaa Gaza inayotumiwa na wanamgambo wa Kipalestina kutengenezea maroketi na kuishambulia Israel. Katika hatua isio ya kawaida Israel ilitangaza operesheni yake hiyo ya ardhini kabla hata ya kuanza.

Njia pekee kuangamiza mahandaki

Waatalamu wanasema operesheni hiyo ya ardhini ni njia pekee ya kufikia maeneo yanayokusudia ambao hayawezi kufikiwa kwa njia ya anga kama vile mtandao huo wa mahandaki. Kabla ya kuanza operesheni hiyo jana usiku, jeshi lilisema lilizima uvamizi wa chini ya ardhi ambapo wanamgambo 13 wa Gaza waliweza kujipenyeza kusini mwa Israel kabla ya kugunduliwa na wanajeshi. Ndege za kivita zilimuuwa mmoja wao na waliobakia wamerudi tena kwenye mahandaki walikotokea.

Mashambulizi ya Israel Gaza wakati wa usiku . (18.07.2014)
Mashambulizi ya Israel Gaza wakati wa usiku . (18.07.2014)Picha: Reuters

Lakini maroketi ya wanamgambo yameendelea kuvurumishwa Israel wakati wa usiku ambapo tisa yameanguka nchini humo na mengine tisa yamedunguliwa hewani.

Hamas kundi lenye kutawala Gaza limesema operesheni hiyo ya Israel itashindwa. Mkuu wa Hamas aliyeko uhamishoni akizungumza kutoka Doha, Qatar, amesema kile ilichoshindwa kufanikisha Israel kwa mashambulizi yake ya anga na baharini haitoweza kufanikisha kwa mashambulizi ya ardhini.

Awali afisa mwandamizi wa Hamas, Osama Hamdan, amesema kundi hilo liko tayari kukabiliana na operesheni hiyo ya ardhini.

Umwagaji damu kuongezeka

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Wapalestina ameonya kwamba operesheni hiyo ya Israel itakuja tu kusababisha kwa umwagaji damu mkubwa zaidi na kuzidi kukwamisha juhudi za kusitisha mapigano.

Majeruhi wa mashambulizi ya Israel Gaza. (18.07. 2014)
Majeruhi wa mashambulizi ya Israel Gaza. (18.07. 2014)Picha: AFP/Getty Images

Uvamizi huo wa Israel unafuatia usitishaji wa mapigano wa muda mfupi kwa misingi ya kibinaadamu na wito wa kidiplomasia wa dharura kwamba Israel iongeze juhudi za kuepusha madhara kwa raia.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameitaka Israel kuweka lengo mahsusi la kupunguza maafa yanayowahusisha raia wasiokuwa na hatia katika mashambulizi yake dhidi ya Gaza.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef