1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaidhinisha ujenzi mpya wa Makaazi ya Walowezi.

Halima Nyanza7 Septemba 2009

Israel leo imeidhinisha ujenzi wa nyumba 455 za walowezi katika eneo la ukingo wa magharibi, hatua ambayo inapingwa na huku wadadisi wakisema ni kikwazo kwa juhudi za kuyafufua mazungumzo ya amani.

https://p.dw.com/p/JVVh
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu. ambaye serikali yake imeidhinisha tena ujenzi wa makaazi ya Walowezi.Picha: AP

Wizara ya Ulinzi ya Israel imethibitisha kuwa Waziri wake Ehud Baraka amesaini kibali hicho cha ujenzi huo wa makaazi.

Kibali hicho cha kuruhuu ujenzi huo, ambacho ni cha kwanza kutolewa tangu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kushika madaraka Machi mwaka huu, kinaonesha jinsi makaazi hayo yanavyoweza kujengwa katika maeneo ambayo Israel inasema inakusudia kuyaweka katika mpango wa baadaye wa amani na Wapalestina.

Nyumba hizo zinatarajiwa kujengwa pia katika maeneo ya kusini na Mashariki mwa Jerusalem na pia katika mji wa Nablus ulioko Ukingo wa Magharibi.

Mjumbe mkuu wa Palestina katika mazungumzo hayo ya kutafuta amani Saeb Erakat amesema uamuzi huo wa Israel unazidi kudhoofisha imani iliyopo kwamba Israel ni wenzao katika kutafuta amani.

Ijumaa iliopita, Maafisa wa serikali ya Israel walitangaza kwamba Waziri Mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu anakusudia kuidhinisha mradi mpya wa ujenzi katika maeneo yaliyotwaliwa, ya Ukingo wa magharibi.

Kibali cha ujenzi huo kilichosainiwa na Waziri wa Ulinzi wa Israel Ehud Barak cha ujenzi wa makazi 455 kinaonesha wazi nchini Israel, kwamba ni jaribio la Bwana Netanyahu kuwatuliza wajumbe wa serikali yake wanaopendelea walowezi na wanachama wa Likud kabla ya makubaliano ya kusimamisha ujenzio huo kuanza.

Bwana Silvan Shalm anamaanisha kuwa wanapaswa kuendeleza mpango huo wa ujenzi wa makazi kwa moyo mmoja na sio nusu nusu.

Bwana Netanyahu, amekubali kusimamishwa kwa muda kwa ujenzi huo lakini sio kusimamisha kabisa katika maeneo yote akisema kwamba lazima kupatikane kwa sehemu za kuishi kwa familia za walowezi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu.

Rais wa Marekani Barack Obama akiongeza matumaini ya nchi za kiarabu kurudisha uhusiano wao wa kawaida na Israel, amekuwa akimshinikiza Waziri Mkuu wa Israel kusimamisha ujenzi huo wa makazi ya walowezi ili kufungua njia ya kuanza tena kwa mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina ambayo yamesimama toka mwezi Desemba mwaka jana.

Akizungumzia tofauti iliyopo kati ya nchi yake na Marekani kuhusiana na mradi huo, Waziri wa Ulinzi wea Israel Ehud Barak alikuwa na haya ya kusema.

Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas amesisitiza kuwa kusimamishwa kwa ujenzi huo wa makazi ya walowezi ndiyo sharti la wao kurudi tena kwenye mazungumzo ya kutafuta amani.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa, Reuters)

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman