1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaimarisha uhusiano na bara la Ulaya

5 Mei 2009

Serikali ya Israel imeonyesha uwezekano wa kuanzisha tena mazungumzo ya kusaka amani ya eneo la Mashariki ya Kati bila ya vikwazo vyovyote.Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu

https://p.dw.com/p/Hk1d
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wa Mambo ya nje Avigdor LiebermanPicha: AP/DPA/DW-Grafik


Hilo limetangazwa wakati ambapo Waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman anafanya ziara rasmi barani Ulaya.Kwa upande uongozi wa kundi la Hamas umesema kuwa uko tayari kuwa sehemu ya kusaka suluhu ya mzozo huo.


Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitangaza hilo kupitia ujumbe mfupi uliotangaziwa kamati ya umma ya masuala ya Marekani na Israel AIPAC kupitia ukanda wa video kutokea mjini Washington.

Waziri Mkuu Netanyahu hata hivyo hakufafanua kinagaubaga suala la kuundwa kwa taifa la Palestina ila aliwasisitizia wajumbe waliokuwa wakihudhuria kikao hicho cha AIPAC kwamba kuna haja ya kuwa na mwanzo mpya katika mchakato mzima wa kusaka amani ya kudumu ya eneo la Mashariki ya Kati.


Israelische Tageszeitung Haaretz
Gazeti la Israel la kila siku la HaaretzPicha: AP

Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la Haaretz kiongozi huyo alisema kuwa Israel inataka kushirikiana na ulimwengu wa mataifa ya Kiarabu vilevile kuwa na amani na Palestina.

Bwana Netanyahu alieleza kwamba anamiini kuwa amani inaweza kupatikana kwa kutumia mazungumzo yanayojikita katika masuala ya kisiasa,kiuchumi na usalama.

Akifafanua hayo Waziri Mkuu Netanyahu alisema kuwa kisiasa mazungumzo hayo sharti yaanze tena haraka iwezekanavyo bila vikwazo vyovyote,kiuchumi Israel iko tayari kuondoa vikwazo vyovyote vitakavyorudisha nyuma juhudi za kuimarisha uchumi wa Palestina.Hata hivyo Kiongozi huyo alisisitiza kuwa usalama wa Israel ni jambo la msingi na Palestina haina budi ila kuitambua Israel kama taifa la Kiyahudi.


Hamas kwa upande wao walipokea kauli hizo kwa kusisitiza kuwa kundi lao liko tayari kuwa sehemu ya kutafuta suluhu ya mzozo huo wa Mashariki ya Kati.Kwa mujibu wa kiongozi wa kisiasa wa Hamas Khaled Meshal aliyehojiwa na gazeti la New York Times,kundi la Hamas limeshasitisha ufyatuaji wa makombora kutokea Ukanda wa Gaza yanayowalenga wakazi wa eneo la kusini mwa Israel.Meshal aliongeza kuwa kundi lake liko tayari kuunga mkono hatua ya kuwa na mataifa mawili ya Israel na Palestina.


Waziri Mkuu Netanyahu pamoja na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas wanatarajiwa kukutana na Rais Obama wa Marekani baadaye mwezi huu.


Italien Israel Außenminister Avigdor Lieberman in Rom bei Franco Frattini
Waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman(kushoto) alipokutana na mwenzake wa Italia Franco Frattini(kulia)Picha: AP

Wakati huohuo Waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman anafanya ziara rasmi ya kwanza tangu kushika wadhifa huo.Ziara hii ina azma ya kubadili sura ya serikali yake katika jamii ya kimataifa.Bwana Lieberman alisisitiza kuwa nchi yake iko tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa kusaka amani ya kudumu ya eneo la Mashariki ya Kati.


Waziri Lieberman alianza ziara yake rasmi hapo jana nchini Italia alikosisitiza ujumbe huo pamoja na suala la mpango wa nuklia wa Iran alilolielezea kuwa jambo linaloutia wasiwasi ulimwengu.Kiongozi huyo anatarajiwa kuzuru pia mataifa ya Ufaransa,Jamhuri ya Czech na Ujerumani kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya Israel na bara la Ulaya. Kulingana na gazeti la Yedioth Ahronoth Lieberman alikutana na mwenzake wa Italia Franco Frattini aliyemhimiza kubadili kauli zake kuhusiana na suala hilo.


Liberman anafahamika kwa kutoa kauli kali ambazo zinaripotiwa kuwaghadhabisha waarabu wachache nchini Israel.Hata hivyo Lieberman alikitetea chama chake kwa kueleza kuwa serikali yake ambayo imekuwa madarakani kwa kipindi cha miezi mitano iliyopita bado kinajiandaa katika sera zake za diplomasia.


Mwandishi:Thelma Mwadzaya AFPE/RTRE

Mhariri:Othman Miraji