1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaimarisha usalama kufuatia mauaji ya waisraeli wanane

Charo, Josephat7 Machi 2008

Rais George W Bush aiongoza jumuiya ya kimataifa kuyalaani mauaji

https://p.dw.com/p/DKMF
Madaktari wa Israel wakiitoa maiti kutoka eneo la mauaji mjini JerusalemPicha: AP

Israel imeimarisha usalama mjini Jerusalem hii leo kwa hofu ya kuzuka machafuko baada ya mpalestina aliyekuwa amejihami na bunduki kuwaua watu wanane katika shule mashuhuri ya kiyahudi mjini humo.

Idadi kubwa ya maafisa wa polisi wa Israel wanashika doria mjini Jerusalem hii leo kufuatia mauaji ya watu wanane yaliyofanywa na mshambulizi wa kipalestina jana usiku. Waisraeli wengine kumi walijeruhiwa katika shambulizi hilo, saba kati yao wakiwa wamelazwa hospitalini. Mshambuliaji huyo alipigwa risasi na kuuwawa na afisa wa jeshi la Israel anayeishi karibu na shule hiyo, na ambaye pia alisoma na kufuzu katika shule hiyo.

Shambulizi hilo dhidi ya wanafunzi wa shule ya Merkaz Harav Yeshiva magharibi mwa Jerusalem, ni la kwanza mjini Jerusalem tangu tarehe 29 mwezi Januari mwaka 2004 wakati waisraeli 19 walipouwawa katika shambulizi la bomu dhidi ya basi mjini humo.

Wakaazi wa kitongoji cha Jabel Mukabaer katika eneo la Jerusalem Mashariki wamesema mshambuliaji huyo ni Alaa Abu Dhein kijana wa miaka 20, ambaye aliwahi kufanya kazi katika shule hiyo ya kidini. Familia ya Abu Dhein imejenga hema la maombolezo na kuweka bendera za kijani za kundi la Hamas nje ya makazi yao. Kijana huyo alikamatwa na polisi wa Israel miezi minne iliyopita lakini akaachiwa miezi miwili baadaye. Polisi wamewatia mbaroni baadhi ya jamaa za kijana ili kuwawahoji.

Polisi wamewekwa katika hali ya tahadhari kote nchini na wameweka vizuizi katika barabara zinaoingia katikati ya miji. Jeshi la Israel limesema limeifunga miji ya Judea na Samaria katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan.

Kundi la Hamas linalolidhibiti eneo la Ukanda wa Gaza limelipongeza shambulio hilo dhidi ya wanafunzi wa kiisraeli likilitaja kuwa kitendo cha kishujaa, lakini likasita kudai kuhusika na mauaji hayo. Wakaazi wa Gaza wameshangilia wakiichukulia hujuma hiyo kuwa kitendi cha kulipa kisasi mauaji ya wapalestina zaidi ya 120 waliouwawa na jeshi la Israel wakati wa harakati ya hivi karibuni, nusu kati yao wakiwa raia. Lakini balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Dan Gillerman, anasema mauaji hayo si ya kulipiza kisasi.

Israel imelitaja shambulio hilo kuwa mauaji ya halaiki lakini imesema itaendelea na mazungumzo ya amani na rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, ambaye amelilaani vikali shambulio hilo la jana usiku. Hii leo lakini baadhi ya wabunge wa Israel wameitaka serikali iyavunje mazungumzo hayo huku wengine wakipinga.

Shambulizi la jana ambalo huenda likakwamisha juhudi za Marekani kufikia mkataba wa kuundwa kwa taifa huru la Wapalestina, limefanywa baada ya ziara ya waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleeza Rice, ambaye aliwatolea mwito rais Abbas arejee tena kwenye meza ya mazungumzo baada ya kuyasitisha.

Bush aiongoza jumuiya ya kimataifa kuyalaani mauaji

Rais George W Bush wa Marekani, ameiongoza jumuiya ya kimataifa kulaani mauaji hayo ya waisraeli, akiyataja kuwa kitendo cha kinyama na kikatili. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amekilaani pia kitendo hicho.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeshinda kufikia makubaliano kuhusu kulilaani shambulio la mjini Jerusalem. Libya imelipinga azimio lililotayarishwa na Marekani kulitaka baraza hilo lililaani shambulio la mjini Jerusalem kuwa la kigaidi. Katika kikao cha dharura cha baraza hilo kilichoitishwa mjini New York, Libya imetaka hatua ya haki ichukuliwe.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza, David Milliband, amelani mauaji ya waisraeli na kuyaeleza kama mshale unaolenga kuyavuruga mazungumzo ya amani baina ya Israel na Palestina. Waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown amesema mauaji ya mjini Jeusalem hayapaswi kuuvuruga mkondo wa mazungumzo ya amani.

Kiongozi wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, amewasilina kwa njia ya simu na waziri wa kigeni wa Israel, Tzipi Livni, kulilaani shambulio hilo na kutoa rambirambi zake kwa jamii za wahanga na maafisa wa Israel.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Bernard Kouchner, ameyalaani vikali mauaji ya mjini Jerusalem na kutaka mazungumzo yenye lengo la kuunda taifa huru la Wapalestina yafanyike.

Canada nayo imehuzunishwa na kitendo hicho. Waziri wa kigeni wa Canada, Maxime Bernier, ametuma risala za rambirambi kwa jamaa za wahanga na serikali ya Israel, akisema Canada inalaani kwa nguvu zote mauaji hayo ambayo hayana faida yoyote kwa mchakato wa kutafuta amani.