1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yajibu mashambulizi ya Hamas

Lilian Mtono
17 Mei 2018

Jeshi la Israel limesema limefanya mashambulizi kaskazini mwa ukanda wa Gaza kujibu mashambulizi  ya Hamas katika mji wa Sderot, ulioko katika mpaka wa Israel. Mpalestina mmoja alijeruhiwa kiasi katika mashambulizi hayo.

https://p.dw.com/p/2xrxT
Israel Protesten in Gaza
Picha: Getty Images/AFP/M. Hams

Jeshi la Israel limesema limefanya mashambulizi kaskazini mwa ukanda wa Gaza mapema hii leo, ikiwa na hatua ya kujibu mashambulizi  ya Hamas katika mji wa Sderot, ulioko katika mpaka wa Israel. Wizara ya afya ya Gaza imesema, Mpalestina mmoja alijeruhiwa kiasi kutokana na mashambulizi hayo.

Kulingana na jeshi la Israel, mashambulizi hayo yamefanyika masaa kadhaa baada ya vikosi vya Israel kushambuliwa kutokea eneo la Palestina. Jeshi hilo limesema, hakukua na mwanajeshi yoyote aliyejeruhiwa wakati wa makabiliano hayo hapo jana.

Ni mashambulizi yanafanywa siku chache baada ya Wapalestina 60 kuuawa na wanajeshi wa Israel katika eneo la mpaka wa Ukanda wa Gaza wakati walipoandamana. Kulingana na jeshi la Israel hii leo kwamba ndege zake zilishambulia kikosi cha jeshi na eneo la kutengeneza silaha kaskazini mwa ukanda wa Gaza.

Maandamano hayo yalichochewa na hatua ya Marekani kufungua ubalozi wake mjini Jerusalem, na kusababisha machafuko mabaya zaidi kutokea katika eneo hilo tangu vita vya mwaka 2014 kati ya Israel na Hamas. Israel imesema kwamba kundi la Kiislamu la Hamas, ambalo mataifa mengi ya magharibi yanalichukulia kama kundi la kigaidi, limetumia maandamano hayo kama kificho cha kuvunja uzio wa mpaka wa Israel na kujaribu kushambulia raia wa Israel. 

Türkei Erdogan kündigt Neuwahlen an
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan ameulaumu Umoja wa mataifa kwa kushindwa kuzungumzia mauaji hayo.Picha: Reuters/M. Cetinmuhurdar

Hapo jana, rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan aliutuhumu Umoja wa Mataifa kwa kuwa dhaifu kuhusiana na  mauaji yaliyotokea Gaza siku ya Jumatatu wakati Marekani ilipokua ukiufungua ubalozi wake Jerusalem. Erdogan alikuwa akizungumza wakati wa futari mnamo siku ya  kwanza ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na kuongeza kwamba, jumuiya ya kimataifa kwa upana wake imeshindwa kuzungumzia matukio hayo.

Uturuki imekuwa mmoja wa wakosoaji wakubwa wa hatua hiyo.

Nchini Ufilipino, mamia wa raia wameandamana hii leo hadi kwenye ubalozi wa marekani uliopo mjini Manila kupinga mauaji ya Wapalestina 59 katika maandamano hayo ya Gaza, mnamo siku ya Jumatatu. Hata hivyo waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango yaliyoishutumu Marekani, walizuiwa na polisi waliokuwa karibu na ubalozi huo, ambako walichoma bendera ya Marekani na Israel.

Katika hatua nyingine, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu  leo ameutaka Umoja wa Mataifa kupitisha azimio kuhusu Jerusalem, katika wakati ambapo mauaji dhidi ya Wapalestina yakizidisha hali ya  mvutano kati ya Israel na Uturuki. 

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE/APE/AFPE/RTRE.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman