1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yakabiliwa na uchaguzi wa mapema

Kalyango Siraj24 Oktoba 2008

Chama cha Shas chagoma kujiunga na serikali ya Livni

https://p.dw.com/p/FgFq
Tzipi LivniPicha: picture-alliance/ dpa

Chama chenye msimamo mkali nchini Isreal cha Shas kimekataa kuingia katika serikali mpya ya mseto ambayo ilikuwa inaandaliwa na waziri mkuu mteule Tzipi Livni.Hii ni ishara kuwa huenda nchi hiyo ikashuhudia uchaguzi mkuu wa haraka.

Chama cha Shas kimetangaza leo kuwa hakita-jiunga na serikali ya mseto ya Bi Livni.Sababu kuu kinasema madai yake hamekataliwa.

Mkuu wa chama hicho, Eli Yisha, amesema kuwa Livni amekataa kukubali madai ya chama chake,ambayo miongoni mwa mengine, ni kuongeza mgao wa pesa kwa walala hoi. Pia kimemtaka waziri mkuu mteule atoe ahadi kuwa sehemu za mji wa Jerusalem hazitagawiwa wa palestina.

Bi Livni, ambae ndie kiongozi wa sasa wa chama cha Kadima alionya jana kuwa ikiwa atashindwa kuunda serikali ifikapo jumapili, ataitisha uchaguzi wa haraka.

Livni amekuwa akijaribu sana kutafuta kuungwa mkono na vyama vidogovidogo mkiwemo hicho cha Shas,ambacho kawaida kimekuwa, katika kipindi kilichopita, kama nguzo kuu katika juhudi za kuundwa kwa serikali za mseto za Israel.

Wiki iliopita chama cha Kadima, ambacho kina viti 29 katika bunge lenye viti jumla 120,kiliafikiana kushirikiana na chama cha Labour kilicho na wabunge 19.

Lakini majadiliano na chama cha Shas yamegonga mwamba.Chama cha Shas ndicho cha tatu kwa ukubwa nchini humo kikiwa na wajumbe 12.

Rais Shimon Perez alimuomba Livni kuunda serikali baada ya kuchaguliwa kuongoza chama cha Kadima kufuatia kujiuzulu kwa Ehud Olmert ili akabiliane na madai ya rushwa.

Licha ya kuombwa kuunda serikali tangu Septemba 22,hadi sasa Livni ameshindwa kutekeleza jukumu alilopewa.

Mchambuzi wa masuala ya siasa katika chuo kikuu cha Tel Aviv, Gideon Doron, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa kimsingi Livni anaweza akaunda serikali ya wachache yenye viti 60.Hata hivyo atahitaji kuungwa mkono na wabunge waarabu,kitu ambacho kinapingwa na baadhi ya wanachama wake.

Endapo Livni atashindwa kuunda serikali hadi jumapili,basi uchaguzi mkuu wa haraka utaitishwa na kura za maoni zinaonyesha kama chama cha Likud kinaweza kujinyakulia ushindi. Pia uchaguzi mkuu utaidumbukiza Israel katika vurugu za kisiasa na kutishia mazungumzo ya amani yanayoendelea kati yake na wa Palestina.