1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yakiri makosa kuhusiana na jamii ya Waethiopia

4 Mei 2015

Israel imekiri kufanya makosa kuhusiana na jamii ya Waethiopia ambapo maelfu ya Waisrael wenye asili ya Ethiopia na wafuasi wameandamana Jumapili (04.05.2015)kupinga ukatili wa polisi na ubaguzi.

https://p.dw.com/p/1FJxO
Maandamano ya Waisrael wenye asili ya Ethiopia Tel Aviv . (04.05.2015)
Maandamano ya Waisrael wenye asili ya Ethiopia Tel Aviv . (04.05.2015)Picha: Reuters/Baz Ratner

Waandamanaji hao walikuwa wakiandamana katika makutano ya barabara kuu mbele ya ofisi za serikali mjini Tel Aviv ambao ni mji mkuu wa kibiashara nchini humo na baadae waliifunga barabara kuu ya Ayalon ambayo ni kiungo kikuu cha usafiri nchini humo na kusababisha msongamano mkubwa wa magari wakati wa kipindi cha harakati za maisha.

Waandamanaji walikuwa wakipiga mayowe, kauli mbio yao ikiwa " hatutaki tena ukatili", "hatutaki ukatili wa polisi" na "tunataka haki sawa ,tunataka kuwa na sauti sawa".

Maandamano hayo yamechochewa kutokana na kuibuka kwa ukanda wa video wenye kuonyesha polisi wawili huko Holon kusini mwa Tel Aviv wakimpiga mwanajeshi wa Israel mwenye asili ya Ethiopia kwa kile kinachoonekana bila ya kuwepo kwa ishara ya shari kutoka kwa mwanajeshi huyo.

Siku moja baadae mkaguzi wa manispaa alimpiga kijana mmoja wa Ethiopia anayeishi kusini mwa Tel Aviv baada ya kumdhania kwa makosa kuwa ni mhamiaji haramu kutoka Eritrea.

Israel imefanya makosa

Rais wa Israel Reuven Rivlin amekiri leo hii kwamba Israel imefanya makosa kwa namna ilivyokuwa ikiishughulikia jamii ya Wayahudi wenye asili ya Ethiopia nchini humo na kuelezea shida zao kuwa ni donda lililo wazi.

Rais Reuven Rivlin wa Israel.
Rais Reuven Rivlin wa Israel.Picha: AFP/Getty Images/M. Kahana

Amesema katika taarifa kwamba wamefanya makosa hawakuwaangalia na kuwasikiliza vya kutosha. Awali rais huyo ambaye wadhifa wake ni wa heshima tu nchini humo na hana mamlaka ya utendajji amelaani maandamano hayo ya jana lakini amekiri kwamba waandamanaji wana manug'uniko ya haki.

Rivlin amesema "Maandamano ni zana muhimu katika demokrasia lakini ghasia sio njia sahihi ya kupata ufumbuzi na wala sio ufumbuzi.Waandamanaji na polisi wamejaribu kuchukuwa hatua za kujizuwiya jambo ambalo linafaa kutiliwa maanani.Tusikubali kuliachia kundi ndogo la fujo lizime kilio cha haki."

Netanyahu ajaribu kutuliza hali

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu leo amekutana na mwanajeshi wa Israel mwenye asili ya Ethiopia mwenye umri wa miaka 19 ambaye kupigwa kwake na polisi ndiko kulikochochea maandamano hayo.

Maandamano ya Waisrael wenye asili ya Ethiopia Tel Aviv . (04.05.2015)
Maandamano ya Waisrael wenye asili ya Ethiopia Tel Aviv . (04.05.2015)Picha: Reuters/Baz Ratner

Alimkumbatia mwanajeshi huyo na kumweleza kwamba alifadhaishwa na kitendo hicho na kwamba kuna mambo yanayohitaji kufanyiwa mabadiliko.

Netanyahu pia anatarajiwa kukutana na viongozi wa jumuiya ya Wayahudi wenye asili ya Ethiopia.

Takriban polisi 46 na waandamanaji 12 walijeruhiwa katika maandamano hayo na watu 43 wametiwa mbaroni.Maelfu ya Wayahudi wa Ethiopia walisafirishwa kuingizwa Israel katika operesheni za siri katika miaka ya 1980 na 1990 jamii yao inayofikia 135,500 kati ya watu milioni nane wa Israel kwa muda mrefu imekuwa ikilalamika kutengwa, kubaguliwa katika kupatiwa elimu na nyumba pamoja kuishi katika hali ya umaskini.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri : Gakuba Daniel