1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yalaumiwa vikali kwa kumkatalia ruhusa waziri wa serikali kuu ya Ujerumani kuingia Gaza

Oumilkher Hamidou21 Juni 2010

Waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani Dirk Niebel asema Israel yafanya kosa kubwa la kisiasa na kwamba haiwarahisishii hata marafiki zake kuweza kuelewa kile wakifanyacho

https://p.dw.com/p/NyQI
Waziri wa misaada ya maendeleo Dirk Niebel akifungua mradi unaogharimiwa na benki ya maendeleo ya Ujerumani huko Nablus-katika Ukingo wa Magharibi wa mto JordanPicha: picture alliance / dpa

Waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani Dirk Niebel anafanya ziara ya siku nne tangu ijumaa iliyopita,nchini Israel na katika maeneo ya utawala wa ndani wa Palastina.Mbali na Ukingo wa magharibi wa mto Jordan,waziri huyo wa misaada ya maendeleo alikua pia afike ziarani Gaza-serikali ya Israel lakini imemkatalia maombi yake hayo.

Uamuzi wa serikali ya Israel kumkatalia ruhusa waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani-Dirk Niebel kuingia katika maeneo ya ukanda wa Gaza umesababisha kutolewa lawama kali kutoka kwa mwanachama wa serikali ya Ujerumani.Inaonyesha kwamba serikali mjini Jerusalem inahofia hali ya uwazi amejibu waziri Niebel:

"Mie nnaona haya ni makosa makubwaya siasa ya nje yanayofanywa na serikali ya Israel .Kwasababu,kwa wakati huu hasa ambapo Israel imetangaza kutaka kubadilisha sera zake kuelekea Gaza,kwamba wanataka kurahisisha bidhaa na pia safari za watu kuingia Gaza,ingekua vyema kutoa ishara tangu sasa.Ningependelea hii ingekua ishara ya kuacha milango wazi na kuanzisha hali ya uwazi.Baadhi ya wakati Israel haifanyi mambo kuwa rahisi kwa hata rafiki yake kuweza kuelewa kile wanachotenda na jinsi wanavyotenda."

"Kosa kubwa la siasa ya nje-kwa lugha ya wanadiplomasia inamaanisha jibu kali na lawama bayana.Hadi dakika ya mwisho wizara ya misaada ya maendeleo imejaribu kuitanabahisha serikali ya Israel-lakini hawajafanikiwa.

Israel Hilfsgüter Grenzblockade
Mtumishi wa kiisrael akinyanyua mfuko wa msaada wa kiutu wa Umoja wa mataifa uliokusudiwa Gaza.Israel inapanga kuregeza makali ya vizuwuzi dhidi ya GazaPicha: AP

Waziri mkuu wa Palastina Salam Fayad nae pia amevunjika moyo.Amesema kupitia kituo kimoja cha matangazo cha Ujerumani tunanukuu:"ikiwa waziri wa Ujerumani anakataliwa ruhusa ya kuingia Gaza-basi hapo bila ya shaka kuna tatizo.Israel si imesema inataka kuregeza makali ya vizuwizi huko Gaza".Mwisho wa kumnukuu waziri mkuu wa Palastina Salam Fayad anaetaka vizuwizi viondoshwe ili bidhaa ziweze kuingia na kutoka katika eneo hilo-njia pekee ya kuinua shughuli za kiuchumi anasema.

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Israel inyonyesha kustaajabishwa na lawama za waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani.Maafisa wanazungumzia juu ya siasa dhahir inayofuatwa na ambayo hairuhusu mwanasiasa yeyote wa ngazi ya juu kuingia Gaza.Katika miezi ya nyuma katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton walikataliwa pia ruhusa ya kuingia Gaza.Jana jumapili baraza la usalama la Israel likiongozwa na waziri mkuu Benjamin Netanyahu limeidhinisha uamuzi wa kupunguza makali ya vizuizi vinavyoikaba Gaza tangu miaka kadhaa iliyopita.

Mwandishi:Grabenheinrich,Christoph/Israel (RBB)/ Hamidou, Oummilkheir

Mpitiaji:Mohammed Abdul-rahman