1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yalegeza mashambulizi yake Gaza kwa saa 3 kwa siku.

Eric Kalume Ponda7 Januari 2009

Wanajeshi wa Israel wameanza kutekeleza mpango wa kusitisha mashambulizi kwa muda wa masaa 3 kwa siku kutoa nafasi ya huduma za kibinadamu kuwafikia zaidi ya Wapalestzina 1.5 katika eneo la Gaza:

https://p.dw.com/p/GTub
Barabara kuelekea Gaza, baada ya wanajeshi wa Israel kusimamisha vita kwa masaa 3.Picha: AP


Vituo vya eneo la mpakani baina ya Gaza na Misri vilifunguliwa kwa mara ya kwanza leo tangu mapigano hayo yaanze disemba 27 mwaka uliopita, huku juhudi za kimataifa zikiendelea katika kujaribu kuutanzua mzozo huo.


Hatua hiyo imetokea huku baraza la mawaziri la Israel likiripotiwa kwamba huenda likaridhia mpango wa amani uliopendekezwa na Misri wa kusitisha mashambulizi.


Baraza hilo la mawazili lilikutana kujadili a suala la iwapo jeshi la Israel liimarishe mashambulizi na kupeleka wanajeshi zaidi ndani ya Gaza au kukubali pendekezo la mpango wa amani lililotolewa jumanne na rais wa Misri Hosni Mubarak na mwenzake wa Ufaransa Nicholas Sarkozy, la kusitisha mapigano kwa muda wa masaa 48,ili kutoa nafasi ya misaada ya kibinadamu kwa wakazi milioni 1.5 wa Gaza.


Viongozi hao wawili walisema kuwa hatua hiyo ni ya muda huku juhudi zikiendelea kupatikane amani ya kudumu katika enreo hilo.


Pendekezo hilo lilitolewa kwa pande zote mbili, ingawa Hamas wanasema kuwa bado wanahitaji muda kabla ya kutoa mapendekezo yao.

Eeneo hilo la Gaza linaripotiwa lilishuhudia hali ya utulivu kwa muda huo wa masaa matatu, baada ya Hamas pia kusitisha mashambulizi yao ya mizinga dhidi ya maeneo ya Israel.Wafuasi hao wa Hamas wametangaza kuwa pia hawataishambulia Israel katika muda huo,mradi tu Israel idumishe ahadi yake.


Mara tu baada ya mpanmgo huo kuanza kutekelezwa, zaidi ya malori 80 yanayosafirisha misaada ya kibinadamu na lita 460,000 za mafuta yaliruhusiwa kuvuka kituo cha mpakani baina ya Misri na Gaza.


Hata hivyo bado haijabainika mpango huo huo utatekelezwa kwa muda Gani.


Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Condolezza Rice alipongeza hatua hiyo na juhudi zinazofanywa kusulughisha mzozo huo, akisema kuwa kinachohitajika ni amani ya kudumu katika eneo hilo la Mashariki ya kati.

Mashambulizi makali yaliendelea leo kabla ya kuanza kwa mpango huo ambapo wanajeshi wa Israel walishambulia jumla ya vituo 40 vinavyodaiwa kutumiwa na Hamas kurusha mizinga ya roketi nchini Israel.


Hali kadhalika msemaji wa jeshi hilo alitoa taarifa kusema kwamba wanajeshi hao pia walishambulia mahandaki na njia za chini ya ardhini zinazotumiwa na Hamas kuendeleza mashambulizi yao.


Kwa kujibu mashambulizi hayo wafuasi wa Hamas pia walirusha jumla ya mizinga 40 ya roketi ndani ya Israel na kuwauwa raia watatu na mwanajeshi mmoja.


Maafisa wa huduma za afya katika ukanda wa Gaza wanasema kuwa zaidi ya Wapalestina 675 wameuliwa huku wengine wasiopungua 3,000 kujeruhiwa.

Baraza la Usalama la umoja wa mataifa bado halijaafikia maamuzi muafaka kukomesha vita hivyo huku mjumbe maalum wa umoja huo katika eneo la mashariki ya kati John Gigs akiitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kukomesha mashambulizi hayo..


Wakati huo huo Rais wa mataifa ya Umoja wa Ulaya Mirek Topolanek umepongeza hatua hiyo ya Israeln kwa kukubali mpango huo ulioafikiwa kwa juhudi za Umoja wa Ulaya na Misri akisema kuwa ni mwelekeo ufaao wa kuwaepushia mateso raia wengi wa eneo hilo wasio na hatia.


Wanajeshi wa Israel waliingia Gaza mwishoni mwa wiki iliyopita kwa mashambulizi ya ardhini baada ya mashambulizi mengine ya angani yaliyodumu kwa muda wa wiki moja, katika juhudi za kuangamiza kabisa uwezo wa kijeshi Hamas kuishambulia Israel.