1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yalegeza vizuizi dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Halima Nyanza17 Juni 2010

Israel imeidhinisha mpango wa kupunguza vizuizi vyake ilivyoweka dhidi ya Gaza, kufuatia wiki kadhaa ambapo nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na shinikizo kimataifa kulegeza vizuizi hivyo.

https://p.dw.com/p/Nt0t
Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.Picha: AP

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Israel imesema kulingana na mpango huo, Israel italegeza mfumo ambao bidhaa za kiraia zitaingia Gaza na kuongeza uingizaji kwa wingi wa malighafi kwa ajili ya miradi ya kiraia ambayo iko chini ya usimamizi wa kimataifa.

Hata hivyo imesisitiza kuwa Israel itaendelea kuimarisha ulinzi ili kuepukana na uingizaji kwa wingi silaha na malighafi nyingine za kutengenezea silaha za kivita katika ukanda huo wa Gaza.

Uamuzi huo wa halmashauri ya mawaziri wanaohusuika na masuala ya usalama katika serikali ya Israel umekuja wakati ambao Jumuia ya kimataifa ikiitolea miito nchi hiyo kulegeza vizuizi ilivyoweka kwa miaka minne  katika mamlaka ya Palestina, ikiwa ni wiki chache tu baada ya kutokea shambulio la umwagaji damu lililofanywa katika meli iliyokuwa ikipeleka misaada Gaza Mei 31, ambapo wanaharakati tisa waliuawa.

Mpango huo ulioidhinishwa leo umeripotiwa kujikita zaidi katika muafaka uliofikiwa  katika siku za hivi karibuni kati ya Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mjumbe maalumu katika kusuluhisha mgogoro wa mashariki ya kati Tony Blair ambao unatoa wito wa kubadili orodha ya vitu vilivyoruhusiwa kuingizwa Gaza na kugeuzwa kuwa orodha ya bidhaa zilizopigwa marufuku.

Itaruhusu pia kuingizwa kwa malighafi nyingi za ujenzi katika miradi ya ujenzi inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa.

Wakati Israel ikitoa uamuzi huo, Jumuia ya Wayahudi wa Ujerumani wameelezea nia yao ya kutaka kutuma meli ya misaada ukanda wa Gaza na kuongezea kuwa hatua yao hiyo haina lengo la kuwasaliti Wayahudi.

Katika mahojiano yake na Shirika la Habari la Ujerumani la -dpa- kiongozi wa jumuia hiyo Kate Katzenstein-Leiterer amesisitiza kuwa wanataka kuonesha kuwa sera ya sasa ya Israel inamakosa, huku nia yao ikiwa ni kutaka nchi hiyo itambulike kama taifa la kidemokrasia dhidi ya hali inayoonekana sasa kama taifa la kihalifu.  

Katika hatua nyingine, Rais Bashar al-assad wa Syria amesema serikali ya Israe inaongeza hatari ya kuzuka kwa vita katika eneo hilo kufuatia shambulio lake la hivi karibuni dhidi ya meli ya misaada.

Amesema tukio hilo limethibitisha kuwa serikali ya Israel inapenda kuchochea moto na kwamba amani haitafikiwa na serikali kama hiyo.

Mwandishi: Halima nyanza(dpa.afp)

Mhariri;Abdul-Rahman