1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yapuuza wito wa kusitisha mapigano

Thelma Mwadzaya6 Januari 2009

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ameitaka Israel jana kusitisha vita vyake dhidi ya ukanda wa Gaza, lakini waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert amepuuzia hatua yoyote ya kusitisha mapigano

https://p.dw.com/p/GSob
Majeshi ya Israel yakishambulia Ukanda wa GazaPicha: AP

Sarkozy alikutana na Ehud Olmert baada ya kukutana na rais wa Palestina Mahmoud Abbas na rais wa Misri Hosni Mubarak , kiongozi aliyefanikisha makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyodumu kwa muda wa miezi sita ambayo muda wake ulimazika Desemba 19 mwaka jana na kuzusha tena matukio kadhaa ambayo yamesababisha uvamizi wa Israel katika Gaza.

Sarkozy amesema baada ya kukutana na Abbas kuwa,mataifa ya Ulaya yanataka kusitishwa kwa mapigano haraka iwezekanavyo. Muda unakwenda mbio dhidi ya amani, amesema Sarkozy . Mapigano lazima yasitishwe na lazima kuwe na makubaliano ya muda ya kiutu ili kusitisha mapigano. Sarkozy akaongeza.''Iwapo Ulaya haitachukua jukumu lake katika kutafuta amani katika mashariki ya kati, hakuna atakayechufanyia.''


Lakini jibu la Ehud Olmert ni kwamba , matokeo ya operesheni inayofanyika hivi sasa katika Ukanda wa Gaza ni lazima yawe kwamba sio tu Hamas waache kurusha makombora lakini pia wasiwe na uwezo kabisa kufanya hivyo.

Hatuwezi kukubali maridhiano ambayo yataruhusu Hamas kurusha makombora kwa muda wa miezi miwili katika miji ya Israel ameeleza waziri mkuu huyo kupitia ofisi yake.

Wanadiplomasia wamesema kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikuwa lifanye mkutano wa ngazi ya mawaziri hii leo kujadili wito wa mataifa ya Kiarabu wa kusitishwa mara moja kwa mapigano na kuwapa ulinzi raia wa Palestina.

Lakini waziri mkuu wa Israel amesema kuwa kwa wakati huu na kutokana na hatua zinazochukuliwa za kidiplomasia , haitakuwa busara kupitisha azimio la Baraza la Usalama kuhusiana na suala hilo, kwasababu uzoefu umeonyesha kuwa Israel haiwezi kumudu kupoteza uhuru wake kwa vitendo vya kigaidi.

Lakini Waziri wa Mambo ya kigeni wa Ufaransa Bernard Kouchner ametahadharisha kuwa hali ya mapigano inazidisha matatizo katika eneo la Mashariki ya Kati.''Ni kweli kwamba mapigano hayo yamesababishwa na uchokozi wa Hamas, lakini kiwango cha Israel ilivyojibu ni kikubwa mno na haiwezi kuvumilika.''


Wakati huohuo wanadiplomasia kutoka mataifa kadhaa ya kusini mwa dunia yako karibu na kulipeleka suala hilo la uvamizi wa Israel katika Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kutokana na kukatishwa tamaa na Baraza la Usalama la Umoja huo kutofanya lolote kuhusiana na kuharibika kwa hali katika ukanda wa Gaza.