1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaridhia kura ya maoni kuamua juu ya maeneo inayoyakalia

23 Novemba 2010

Bunge la Israel limepitisha muswada unaoungwa mkono na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu unaohitaji kuwepo kura ya maoni kuhusu uwezekano wa kuyarudisha maeneo inayoyakalia kimabavu ili kurejesha amani Mashariki ya Kati

https://p.dw.com/p/QFrW
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin NetanyahuPicha: picture alliance / dpa

Muswada huo uliopitishwa baada ya majadiliano yaliyodumu kwa muda wa saa saba kwa kura 65, huenda yakayafanya mazungumzo kati ya Israel na Palestina ambayo yanaungwa mkono na Marekani kuwa magumu zaidi. Mazungumzo hayo yamekwama kwa wiki kadhaa sasa kutokana na suala la ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi. Wabunge 33 walipiga kura ya kuukataa muswada huo.

Maale Adumim Siedlung Osten Jerusalem
Sehemu ya Jerusalem MasharikiPicha: Stephanie Gebert

Hata hivyo, mpatanishi mkuu wa Palestina, Saeb Erakat, amekemea uamuzi huo wa bunge la Israel, akisema kuwa umepuuza sheria za kimataifa na kuyataka mataifa kulitambua eneo la Ukingo wa Magharibi kama sehemu ya taifa la Palestina, eneo ambalo lilitwaliwa na Israel  katika vita vya mwaka 1967.

Sheria ya Israel inataka umma kuamua iwapo kuwe na mkataba wowote utakaojumuisha kuondoka kwa Israel katika maeneo yanayoyakalia kwa mabavu, katika tukio ambalo bunge la Israel linahitaji kuunga mkono muswada huo kwa theluthi-mbili ya kura, ili uweze kuwa sheria.

Mkataba huo utajumuisha Israel kuondoka katika maeneo ambayo inayakalia kwa mabavu ya Jerusalem Mashariki au eneo la milima ya Golan ambalo walilichukua kutoka Syria. Erakat amesema Israel inalazimika kuondoka katika maeneo hayo bila kujali matokeo yatakayopatikana baada ya wananchi watakapopiga kura ya maoni.

Wapalestina wanataka Jerusalam Mashariki uwe mji wao mkuu wa taifa lao la baadae, lakini Israel inaliona eneo hilo kama sehemu ya eneo la mji wake mkuu usiogawanyika na huenda ikawa vigumu kuwashawishi wananchi wa Israel kuunga mkono muswada huo. Viongozi wa Palestina pia wamesema kuwa wanatarajia kufanya kura ya maoni katika mkataba wowote ule na Israel.

Katika taarifa yake, Bwana Netanyahu amepongeza uamuzi huo wa bunge wa kufanyika kura ya maoni ndani ya siku 90, ili kupunguza mivutano na wasiwasi. Waziri huyo mkuu wa Israel pia amesema ana imani Waisraeli wataunga mkono makubaliano ya amani kwa maslahi ya kitaifa na mahitaji ya usalama wa nchi hiyo.

Mtaalamu wa sayansi ya siasa katika chuo kikuu cha Tel Aviv, Orit Galili-Zucker, amesema kuwa faida za kura hiyo ya maoni huenda ikazishinda hasara zake na kwamba Bwana Netanyahu anaweza akaitumia kama njia ya kupata ushindi mkubwa katika kuwepo kwa mkataba huo. Wachambuzi wengine wa kisiasa wanadhani kuwa kura hiyo ya maoni inaweza kuendeleza kukwama kwa masuala ya kidiplomasia.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Franco Frattini baadae leo atafanya mazungumzo yake katika siku ya pili na maafisa wa Israel na Palestina.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE)

Mhariri: Miraji Othman