1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yasema haina mgogoro na Marekani, huku EU ikiitaka kuachana na ujenzi wa makaazi.

Halima Nyanza22 Julai 2009

Balozi mpya wa Israel nchini Marekani amesema hakuna mgogoro wowote kati ya nchi yake na Marekani, licha ya kupingana kuhusiana na ujenzi wa makaazi katika Mashariki mwa Jerusalem.

https://p.dw.com/p/Iv6r
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambaye nchi yake inalalamikiwa kuendelea na ujenzi wa Makaazi ya walowezi, mashariki mwa Jerusalem.Picha: AP

Balozi Michael Oren ameiambia Radio ya Israel kwamba hakuna mgogoro wowote katika uhusiano wa Israel na Myarekani, na kwamba wamekuwa wakijadiliana tu kuhusiana na kutokubaliana kwao juu ya masuala fulani.


Mahojiano hayo yamefanyika kufuatia ripoti kwamba Marekani na Israel zimekuwa katika mgongano juu ya msimamo wa Israel wa kuendelea na ujenzi wa makazi hayo ya walowezi.


Marekani imekuwa ikiitaka Israel kusitisha shughuli zake hizo.

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel alisema kuwa wakati Israel haijengi makazi yoyote mapya au kupokonya ardhi zaidi katika Ukingo wa Magharibi, itaendelea na ujenzi katika makazi yaliyokuwapo kwa ajili ya kukabiliana na ongezeko la watu.


Awali, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilimuita balozi wa Israel nchini humo, Michael Oren, kupata ufafanuizi zaidi juu ya mpango huo wa Israel wa ujenzi wa makaazi katika eneo la mashariki mwa Jerusalem.


Hata hivyo, Balozi Oren ameelezea kuwa na nia njema kati ya nchi hizo mbili katika jaribio la kufikia suluhu ya mjadala huo.

Lakini hakusema ni lini tofauti kati yao itamalizika lakini amefikiri kumalizika karibuni.


Hapo jana Ujerumani, Ufaransa na Rais wa sasa wa Umoja wa Ulaya, Sweden, kwa pamoja ziliungana na mataifa ya magharibi kuishinikiza Israel kusimamisha ujenzi huo wa makazi mashariki mwa Jerusalem na katika Ukingo wa Magharibi, chini ya juhudi zinazoongozwa na Marekani za kuanzisha tena mazungumzo ya amani yaliyozorota.


Mjini Berlin, hapa Ujerumani, mwanachama mwandamizi katika chama cha Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Ruprecht Polenz, amenukuliwa akisema kuwa Israel inajiweka katika hatari ya kujiua yenyewe kama taifa lenye kufuata demokrasia, iwapo halitaachana na ujenzi huo.

Der Vorsitzende des Auswärtigen Ausschusses im Deutschen Bundestag, Ruprecht Polenz
Kiongozi wa Kamati ya Bunge la Ujerumani-Mambo ya Nje, Ruprecht Polenz, amesema Israel inajiweka katika hatari ya kujiua yenyewe, kama taifa lenye kufuata demokrasia iwapoa haitaachana na ujenzi huo wa makaazi.Picha: DPA


Bwana Polenz ambaye anaongoza kamati ya bunge ya mambo ya nje ameliambia gazeti la Rheinische Post la hapa nchini kwamba Israel haitilii maanani ukweli kwamba si Palestina wala Mataifa ya Kiarabu yatakayokubali ufumbuzi wa tatizo hilo bila Jerusalem Mashariki.


Nayo Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa ilimuita balozi wa Israel nchini humo, Daniel Shek, mjini Paris, kupinga mpango huo wa ujenzi wa nyumba mashariki mwa Jerusalem, eneo ambalo Israel inazingatia kwamba ni sehemu ya mji wake mkuu na ambao Wapalestina pia wanataka kuufanya kuwa mji wao mkuu.


Kwa upande wake, Sweden, nchi ambayo kwa sasa ni Rais wa Umoja wa Ulaya, imeitaka Israel kuachana na ujenzi huo.


Mwandishi: Halima Nyanza (dpa, Reuters)

Mharir: Miraji Othman