1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yazidisha mashambulizi ya mabomu dhidi ya Gaza

Iddi Ssessanga
24 Oktoba 2023

Israel imeendeleza mashambulizi dhidi ya Gaza kabla ya uvamizi unaotarajiwa wa ardhini dhidi ya wapiganaji wa kundi la Hamas, huku idadi ya vifo ikiongezeka kwa kasi na wasiwasi juu ya kusambaa kwa mzozo huo ukiongezeka.

https://p.dw.com/p/4XwuG
Ukanda wa Gaza | Moshi ukitanda kufuatia mashambulizi ya Israel
Moshi ukitanda kufuatia mashambulizi ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza, Jumatatu Oktoba 23, 2023.Picha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Vita hivyo ambavyo vimeingia siku ya 18 hii leo, ndiyo vibaya zaidi kati ya vita vitano vya Gaza kwa pande zote mbili. Wizara ya afya inayoongozwa na Hamas imesema Wapalestina wasiopungua 5,087 wameuawa na 15,270 wamejeruhiwa.

Katika eneo linalokaliwa kimabavu la Ukingo wa Magharibi, Wapalestina 96 wameuawa na 1,650 kujeruhiwa katika ghasia na uvamizi wa Israel tangu Oktoba 7.

Zaidi ya watu 1,400 wamuuawa nchini Israel, wengi wao wakiwa ni raia waliofariki katika shambulio la awali la Hamas. Marekani, Umoja wa Ulaya na Ujerumani zimeirodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi.

Aidha, watu 222 wakiwemo wageni wanaaminika kuchukuliwa mateka na Hamas wakati wa uvamizi na kupelekwa Gaza, kulingana na jeshi la Israel. Wanne kati yao wameachiliwa.

Kivuko cha Rafah, Misri | Misaada ya Kiutu ikiingizwa Gaza
Lori lililobeba msaada likiingia Gaza kupitia kivuko cha Rafah upande wa Misri, Oktoba 22, 2023. Shirika la wakimbizi wa Kipalestina la UN, UNRWA, limetoa wito wa kuruhusiwa misaada kuingia Gaza pasina vizuwizi vyovyote.Picha: Ahmed Gomaa/Xinhua/IMAGO

Israel imesema leo kuwa imeuwa wapiganaji kadhaa wa Hamas katika mashambulizi ya usiku, na kwamba haina nia ya kulegeza mashambulizi dhidi ya Gaza.

Soma pia: Mateka wawili waachiwa huru na kundi la Hamas

Shirika la la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi wa Palestina, UNRWA, limetoa wito wa kuruhusiwa kuingia kwa misaada pasina vizuwizi vyovyote, likisema aktika taarifa kwamba malori yalioruhusiwa kuingiza misaada Gaza mpaka sasa ni kama tone tu kwenye bahari.

Marekani pia imeihimiza Israel kuruhusu misaada zaidi kuingizwa Gaza, lakini kumeonekana kuwa na matumaini finyu ya usitishaji mapigano.

Macron: Tunasimama bega kwa bega na Israel

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, alieko ziarani nchini Israel, ameapa kutoiacha Israel katika mapambano yake dhidi ya wapiganaji wa Gaza, lakini ameonya dhidi ya hatari ya mzozo wa kikanda.

Baada ya kukutana na familia za waathirika wa Kifaransa katika uwanja wa ndege wa Tel Aviv, Macron alimuambia rais wa Israel Isaac Herzog mjini Jerusalem, kwamba Ufaransa inasimama bega kwa bega na Israel.

Soma pia: London, Berlin waandamana kupinga chuki kwa Wayahudi, kwengineko kuipinga Israel

"Nataka uwe na uhakika kwamba haujaachwa peke yako katika vita hivi dhidi ya ugaidi. Kwa sababu ninazungumza hapa kwa niaba ya nchi ambayo ilikumbwa na mashambulizi kama hayo ya kigaidi, na ulikuwepo wakati huo," alisema Macron.

Israel, Jerusalem | Rais wa Ufaransa Macron na rais wa Israel  Herzog
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akisalimiana na Rais wa Israel Isaac Herzog baada ya mazungumzo yao mjini Jerusalem, Oktoba 24, 2023.Picha: Christophe Ena/Pool/Reuters

"Na, nadhani huu ni wajibu wetu kupigana na vikundi hivi vya kigaidi, bila mkanganyiko wowote, bila kutanua mzozo huu. Na ninashiriki maonyo uliyotoa. Lakini kulenga makundi haya ya kigaidi, kupanga operesheni zinazolenga hasa wapiganaji ni jambo muhimu."

Soma pia: Fahamu mizani ya kijeshi kati ya Israel na Hamas

Ziara ya Macron imekuja baada ya mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya kupambana jana Jumatatu kukubaliana juu ya wito wa usimamishaji wa muda wa mapigano kwa sababu za kiutu, ili kuruhusu msaada zaidi kuwafikia raia.

Macron pia anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Benjamin Netanyahu, pamoja na viongozi wa upinzani wa mrengo wa kati, Benny Gantz na Yair Lapid, na baadae Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas, kwa mujibu wa taarifa ya ikulu ya Elysee.

Wasiwasi wa kutanuka kwa mzozo

Wakati ambapo kundi linaloungwa mkono na Iran la Hezbollah likifyatuliana maroketi na jeshi la Israel katika mpaka wake na Lebanon, serikali za mataifa ya Magharibi zina wasiwasi kwamba mzozo huo huenda ukatanuka.

Soma pia: Je, uhalifu wa kivita unapimwa vipi kwenye mzozo?

Rais wa Marekani Joe Biden, Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, pia waliibua wasiwasi huo wakati wa ziara zao nchini Israel wiki iliyopita.

Msafara mwingine wa malori ya misaada waingia Gaza

Macron anatazamiwa kutoa wito wa kuwalinda raia wa Gaza katika mazungumzo na Netanyahu, wakati ambapo Israel ikiendeleza mashambulizi mfululizo ikijiandaa na uvamizi unaotarajiwa wa ardhini.

Chanzo: Mashirika