1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israeli na Hezebollah wazungumza juu ya wafungwa

Nijimbere, Gregoire27 Mei 2008

Mazungumzo kati ya Israeli na kundi la Hezebollah la nchini Lebanon juu ya swala zima la kubadilishana wafungwa yamepiga hatua kubwa. Hayo yamethibitishwa na pande zote mbili husika yaani Israeli na Hisibollah.

https://p.dw.com/p/E6nJ
Wanajeshi wa Israeli wakirejea nyumbani kutoka LebanonPicha: AP


Afisa mmoja wa Israeli ambae hakupenda jina lake litajwe amethibitisha kwamba mazungumzo hayo sasa yamefikia kwenye hatua ya kuridhisha na kwamba wanakaribia kufikia mkataba na Hezebollah. Amezidi kusema kuwa mambo yalianza kuenda vizuri kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu. Mpatanishi kutoka Ujerumani Gerhard Konrad alikuwa katika mji mkuu wa Lebanon Beirut wiki jana kuzungumza na kundi la kishiha la Hezebollah na kuhakikisha kwamba pande hizo mbili yaani Israeli na Hisibollah zinakaribia kuwaachia wafungwa wa kila upande.

Hata kundi la Hezebollah limesema watu wake wanakaribia kuachiliwa huru na Israeli.

Kiongozi wa Hezebollah Sheikh Hassan Nasrallah aliyatamka hayo akiuhotubia umati wa wafuasi wake mjini Lebanon hapo jana:


" Kuachiwa kwa wafungwa ni wajibu wetu na ni ahadi tulioitoa. Tutakamilisha huo mchakato wa kuachiwa wafungwa kwa msaada wa Mwenyezi Mungu. Hivi karibuni tu Samir na ndugu yake watakuwa nyumbani Lebanon"


Vyombo vya habari nchini Israeli vimeripoti kwamba Israeli inatarajia kumuachia huru huyo Samir Kantar aliyetajwa na Hassan Nasrallah katika hotuba yake na ambae alikamatwa mwaka 1979 kwa tuhuma za kumuuwa baba na binti wake wakati wa shambulio katika mji wa Nahariya kaskazini mwa Israeli na kukatiwa kifungo cha miaka 542 jela. Wataachiwa pia raia mmoja na wapiganaji wanne wa Hezebollah waliokamatwa wakati wa vita vya zaidi ya mwezi mmoja kati ya Israeli na Hisibollah mwaka 2006.

Ataachiwa pia raia mmoja kutoka Israeli na ambae alikamatwa kwa tuhuma za kulifanyia ujasusi kundi la Hisibollah.

Kwa upande wa Israeli, wanatarajiwa kuachiwa huru wanajeshi wake wawili Ehud Goldwasser na Eldad Regev ambao kukamatwa kwao na Hezebollah kwenye eneo la mpakani mwezi Julai mwaka wa 2006, kulikuwa kiini cha vita vilivyodumu siku 34 kati ya Israeli na Hisibollah.


Mazungumzo hayo kati ya Israeli na Hezebollah juu ya wafungwa hayakuwa rahisi. Ujerumani ilikabidhiwa jukumu la kuongoza majadiliano hayo mara tu baada ya vita kusimama na maendeleo yake kuwa siri hadi hivi karibuni ambapo imefichuliwa kwamba pande hizo mbili zinakaribia kufikia mkataba.

Tukio la hivi karibuni kubadilishana wafungwa kati ya Israeli na Hezebollah lilitokea mwezi Octoba mwaka uliopita ambapo kundi la Hezebollah liliikadhidi Israeli mabaki ya mwanajeshi wake aliyeuliwa huku Israeli ikiitolea Hezebollah mfungwa mmoja pamoja na maiti za wapiganaji wake wawili waliouliwa na Israeli.