1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia Yapata Waziri Mkuu Mpya

Admin.WagnerD24 Aprili 2013

Mkwamo wa wiki 8 katika mchakato wa kuunda serikali ya Italia unaelekea kumalizika, baada ya kuteuliwa kwa Enrico Letta kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo. Uteuzi huo umeyafurahisha masoko na washirika wa kimataifa wa Italia.

https://p.dw.com/p/18Mqc
Enrico Letta, waziri mkuu mpya wa Italia
Enrico Letta, waziri mkuu mpya wa ItaliaPicha: Reuters

Akizungumza baada ya kumteua Enrico Letta kuwa waziri mkuu mpya wa Italia, rais wa nchi hiyo Giorgio Napolitano alisema ''kwa vigezo vya Italia'' kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 46 ni kijana, ambaye hata hivyo amejikusanyia uzoefu wa kutosha katika siasa za nchi hiyo. Enrico Leta amekwishashikilia nyadhifa muhimu, ikiwa ni pamoja na kuwa waziri wa viwanda na biashara ya nje kati ya mwaka 2000 na 2001, na pia naibu waziri katika serikali ya Romano Prodi. Hali kadhalika, Letta alikuwa mbunge katika bunge la Ulaya kati ya mwaka 2004 na 2006.

Majukumu mazito

Letta ameukubali wadhifa huo kwa tahadhari, kwa maana kwamba anataka kwanza kuhakikisha kuwa anao uungwaji mkono wa kutosha bungeni kuhusu baraza la mawaziri atakaloliteuwa, kabla ya kukubali rasmi uteuzi huo. Akizungumza na vyombo vya habari, Letta alisema Italia haiwezi kungoja milele kupata waziri mkuu mpya.

Rais wa Italia Giorgio Napolitano akiwa bungeni
Rais wa Italia Giorgio Napolitano akiwa bungeniPicha: ALBERTO PIZZOLI/AFP/Getty Images

''Hatuwezi kusubiri zaidi. Kwa hiyo nimekubali kuchukuwa majukumu haya, hata kama ni mazito sana kwenye mabega yangu. Nauchukuwa wadhifa huu nikiwa na dhamira kubwa, kwa sababu Italia inahitaji majibu.'' Alisema Letta.

Waziri mkuu huyo mteule wa Italia amesema anakwenda kufanya mashauriano, na atatoa jibu lake kwa rais katika muda mfupi iwezekanavyo. Anategemewa kuunda seriikali ya mseto ambayo itajumuisha chama cha waziri mkuu wa zamani Silvio Barlusconi, PDL, na kundi lenye siasa za mrengo wa kati linaloongozwa na mtangulizi wake, Mario Monti.

Muda wageuka kikwazo

Kikwazo kikubwa katika kuundwa kwa mseto huo kinatokana na mitazamo tofauti juu ya muda ambao serikali ya Enrico Leta itabakia madarakani. Silvio Berlusconi na chama chake cha kihafidhina wanasema kuwa wanataka serikali itakayodumu kwa muda mrefu, huku chama cha PD ambacho kinajiunga shingo upande na serikali hiyo, kikisema kitafanya hivyo tu ikiwa serikali hiyo itakuwa ya muda mfupi.

Enrico Letta anaichukua nafasi iliyoachwa wazi na Mario Monti aliyejiuzulu.
Enrico Letta anaichukua nafasi iliyoachwa wazi na Mario Monti (Pichani) aliyejiuzulu.Picha: picture-alliance/AP Photo

Letta amesema anataka serikali itakayolitumikia vyema taifa, ikiwa na dira inayoeleweka kimaendeleo. Miongoni mwa masuala yenye kipaumbele kwake ni kuunda nafasi za ajira, na kuhamasisha ukuaji wa uchumi. Aidha, amesema ataunga mkono mageuzi katika taasisi za umma, na kuutaka Umoja wa Ulaya ulegeze sera zake ambazo zinajikita zaidi kwenye suala la kujifunga mkanda.

Waziri mkuu huyo mpya wa Italia ameyashughulikia sana masuala ya muungano wa Ulaya. Mnamo miaka ya 1990, aliongoza kitengo cha wizara ya fedha ambacho kiliitayarisha Italia kujiunga na kanda inayotumia sarafu ya Euro. Mojawapo ya majukumu muhimu ya serikali yake ni mazungumzo na Umoja wa Ulaya, ambayo yatajaribu kuuomba umoja huo ulegeze masharti kwa bajeti ya Italia, suala ambalo linaungwa mkono na vyama vingine, vikiwemo DP na PDL cha Barlusconi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/DPAE

Mhariri: Josephat Charo