1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ivory Coast: Upigajikura wamalizika, matokeo yangojewa

Admin.WagnerD29 Novemba 2010

Sasa wapigakura wanasubiri matokea ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais uliofanyika jana (28 Novemba 2010), unaotazamiwa kuleta utulivu katika taifa hilo lililozongwa na msukosuko.

https://p.dw.com/p/QKxq
Mtetezi wa kiti cha urais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo
Mtetezi wa kiti cha urais wa Ivory Coast, Laurent GbagboPicha: picture alliance/PANAPRESS/MAXPPP

Tume ya uchaguzi nchini Ivory Coast imesema imemaliza kuhesabu kura baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa, na kwamba wakati wowote kuanzia leo itatangaza matokeo ya uchaguzi huo.

Rais aliye madarakani Laurent Gbagbo amepata upinzani mkali kutoka kwa Allasane Ouattara, Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni afisa wa Shirika la fedha duniani IMF. Ni upinzani ambao umefufua machafuko na kuanzisha tena wasiwasi katika taifa hilo, ambalo ndio mzalishaji mkuu wa zao la kokoa.

Umma ukimuangalia mgombea urais Alassane Ouattara akizungumza kwenye mdahalo
Umma ukimuangalia mgombea urais Alassane Ouattara akizungumza kwenye mdahaloPicha: dpa

Kulingana na msimamizi wa kampeni ya Rais Gbgabo maafisa watano wa usalama waliuawa magharibi mwa nchi hiyo, muda mfupi tu kabla ya kura kuanza kuhesabiwa. Vyanzo vya habari vya usalama vinasema mauaji hayo yalitokea nje ya vituo vitatu vya kupigia kura, wakati raia waliokuwa na hasira walipolalamika kuwa walizuiawa kupiga kura.

Tangu vita vya 2002-2003 Ivory Coast imegawanyika katika pande mbili, huku waasi wakitawala Kaskazini, hali ambayo imelitua katika hali ya msukosuko taifa hilo la Magharibi mwa Afrika ambalo lilikuwa wakati mmoja lilikuwa kielelezo cha ufanisi wa uchumi.

Duru ya kwanza ya uchaguzi uliotarajiwa kuponesha kidonda hicho, ilifanyika Oktoba 31. Lakini ndio ikawa mwanzo wa kinyanganyiro kikali baina ya wagombea wawili wakuu. Hadi jana kulipofanyika duru hiyo ya pili watu saba wameuawa.

Waangalizi wa uchaguzi huo, walifanya mkutano jana jioni na Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na madai ya kuwepo kwa visa vya udanganyifu.

Kiongozi wa ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulya, Christian Dan Preda aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba kulikuwa na ripoti za barabara kufungwa, wasiwasi katika vituo vya kupigia kura pamoja na uhaba wa vifaa vya kupigia kura ikiwemo makaratasi ya kura. Na hili halikuwa hivyo katika duru ya kwanza alimalizia Preda.

Huku kura zikianza kuhesabiwa, makundi ya wafuasi wa kila mgombea walikusanyika nje ya vituo vingi vya kupigia kura katika mji mkuu Abidjan.

Msimamizi wa kampeini ya Quattara aliwaambia waandishi wa habari kuwa wawakilishi wao walizuia kuingia katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, ilhali wengine walifurushwa kutoka vituo vingine.

Wakati huo huo, msimamizi wa Waziri wa usalama wa ndani nchini humo amewashtumu waasi ambao bado wanaongoza eneo la Kaskazini kwa kuwatolea vitisho wafuasi wa serikali. Msimamizi huyo pia alisema watawasilisha malalamiko yao katika mahakama ya kikatiba.

Mwandishi: Munira Muhammad/ RTRE

Mhariri: Abdu Mtullya.