1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ivory Coast yakamilisha kampeni kwa machungu

Admin.WagnerD26 Novemba 2010

Uchaguzi wa marudio nchini Ivory Coast unafanyika Jumapili ya 27 Novemba 2010, lakini tayari umetiwa doa na machafuko yaliyotokea kwenye kampeni, ambapo kwa uchache yamegharimu roho ya mtu mmoja hadi sasa

https://p.dw.com/p/QJYm
Mtetezi wa kiti cha urais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo
Mtetezi wa kiti cha urais wa Ivory Coast, Laurent GbagboPicha: AP

Jana (26 Novemba 2010), wafuasi wa Laurent Gbagbo, ambaye anatetea nafasi hiyo, na wa mpinzani wake, waziri mkuu wa zamani Alassane Ouattara, walijazana katika viwanja tafauti vya mji mkuu wa Abdijan kuwaunga mkono viongozi wao.

Wakiwa wamevalia fulana nyeupe, maelfu ya wafuasi wa Gbagbo waliandamana kuzunguka uwanja wa Place de la Republique, huku wakiimba. Mmoja wao alibeba bango lililosomeka: "Sasa tuna amani, tumpigie kura Gbagbo."

Wafuasi wa Ouattara nao, walijikusanya kwenye wilaya ya Cocody, Kaskazini Mashariki ya Abidjan, ambako mgombea wao alitarajiwa kuwahutubia.

Kiongozi wa Upinzani na mgombea urais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara
Kiongozi wa Upinzani na mgombea urais wa Ivory Coast, Alassane OuattaraPicha: AP

Kwa ujumla, hali ya kampeni kuelekea jana haikuwa ya kuridhisha, isipokuwa katika tukio moja tu la mdahalo wa ana kwa ana baina ya wagombea hao kwenye televisheni. Ingawa wote walikuwa wakizungumzia umuhimu wa amani, kila mmoja kati yao alikuwa akimlaumu mwenzake kwa kutumia maneno makali ya matusi na kashfa, kama vile kuitana nyoka, waongo na waasi, na wakati huo huo wakiwaomba wapiga kura wasiruhusu nchi yao kuangukia mikononi mwa makatili.

Hali hii ya uhasama ilifikia kilele chake Alhamis iliyopita huko katika mji wa Bayota, wakati mtu anayesadikiwa kuwa mfuasi wa Ouattara, alipomuua mfuasi wa Gbagbo aliyejaribu kuichana picha ya Ouattara.

Lakini mdahalo wa Alkhamis (25 Novemba 2010), ulishuhudia wagombea hao wawili wakitoa kauli za kutia moyo kuliko walivyozoeleka. Gbagbo alisema kwenye mdahalo huo: "Tumekubaliana kukubaliana na matokeo", huku Ouattara naye akisema: "Natarajia kushinda kwa sababu nataka kuisaidia nchi yangu, lakini nikishindwa si tatizo."

Katika mdahalo huo, Gbagbo alisema atatangaza hali ya kutotoka nje watu baada ya upigaji kura kumalizika hiyo kesho, ili kuhakikisha usalama. Gazeti linaloegemea upande wake, Le Temps, lilisifu kauli hiyo kuwa inawahakikishia raia usalama wao, lakini gazeti linalomuunga mkono Ouattara, Le Patriote, liliuita huo kuwa ni mpango wa kuiba uchaguzi.

Gbagbo na Ouattara waliutumia mdahalo wa juzi kistaarabu kuzungumzia masuala ya amani, ajira, umasikini na uchumi na sio kutukanana, jambo lililowaacha wafuasi wao midomo wazi, kama alivyosema kijana wa miaka 25 anayefanya kazi za biashara, Karim Seguena: "Ulikuwa mdahalo wa kupendeza sana. Nimeshangazwa kwelikweli na namna ulivyokuwa wa kistaarabu."

Ggagbo alijipigia kampeni kama kiongozi aliyethibitsha uwezo wake kwa kuipatia nchi amani, huku Ouattara akijielezea kupitia rekodi yake ya kiuchumi alipokuwa afisa wa ngazi za juu kwenye Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF.

Viongozi wa kidini, ujumbe wa Umoja wa Mataifa na wa Umoja wa Ulaya, wamewataka wanasiasa hao kuhakikisha nchi yao haingii tena kwenye machafuko. Vikosi vya Ivory Coast na vile vya Umoja wa Mataifa vimejiweka katika hali ya tahadhari.

Kura hii ya kesho (29 Novemba 2010) inatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa amani, baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2002 kuipasua nchi mapande mawili, baina ya lile la Kusini lenye Wakristo wengi anakotokea Gbagbo; na lile la Kaskazini lenye Waislam wengi anakotokea Ouattara.

Katika kura hii, wote wawili wanapigania kura za aliyekuwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Henri Konan Bedi, ambaye alitokea wa tatu katika uchaguzi wa mwanzo uliofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita. Bedi mwenyewe alishatangaza rasmi kumuunga mkono Ouattara, ambaye alipata asilimia 32 dhidi ya asilimia 38 za Gbagbo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE

Mhariri: Othman Miraj