1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jürgen Klinsmann ana kibarua kigumu

2 Juni 2014

Tangu iliporejea katika Kombe la Dunia mnamo mwaka wa 1990 baada ya kuwa nje kwa miaka 40, Marekani imekuwa ikisajili matokeo tofauti katika awamu ya makundi na hata kuwahi kufuzu katika awamu ya mwondoano.

https://p.dw.com/p/1CAHb
Interaktiver WM-Check 2014 Mannschaft USA
Picha: picture alliance/dpa

Ghana iliwazika kabisa Wamarekani katika duru ya kwanza mwaka wa 2006, kisha miaka minne baadaye, The black Stars wakawazaba katika muda wa ziada na wakafuzu katika duru ya 16 za mwisho.

Mwaka huu, Wamarekani wanafungua dimba dhidi ya timu hiyo hiyo kabla ya kuchuana na Ureno na Ujerumani katika kile kinachoonekana kuwa mojawapo ya makundi magumu zaidi.

Kocha wa Marekani Jürgen Klinsmann anasema hajisi kama wanaelekea Brazil kama timu inayotarajiwa kushindwa. Anasema anahisi kama kuanzia siku ya kwanza watakuwa washindani wakali na anafikiria wachezaji wake wanahisi hivyo.

Kocha Klinsmann aliwashangaza wengi kwa kumwacha nje ya kikosi gwiji Landon Donovan
Kocha Klinsmann aliwashangaza wengi kwa kumwacha nje ya kikosi cha kwenda Brazil gwiji Landon DonovanPicha: Nicholas Kamm/AFP/Getty Images

Klinsmann ambaye ni mshambuliaji wa zamani nyota wa Ujerumani aliyeshinda Kombe la Dunia mwaka wa 1990 na Kombe la Ulaya mwaka wa 1996, alihamia Carlifonia na mkewe Mmarekani baada ya kustaafu kamamchezaji mwaka wa 1998. Wakati alipoifunza Ujerumani na kufika katika nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka wa 2006, alionekana kuwa kocha aliyesubiriwa sana na Marekani na akachukua usukani miaka mitatu iliyopita kutoka kwa Bob Bradley.

Klinsmann aliwaongoza Wamarekani kwa kunyakua taji la kwanza la CONCACAF Gold Cup na kufuzu kwa mara saba mfululizo katika Kombe la Dunia. Amefanya uamuzi wa wenye utata wa kumwacha nje ya kikosi chake Landon Donovan mwenye umri wa miaka 32, ambaye anaongoza kwa kuifungia Marekani magoli 57.

Tim Howard anarejea kutoka kwa mwaka wa 2010 kama mlinda lango nambari moja na ana ujuzi wa misimu mianne kama kipa wa kikosi cha kwanza katika timu yake ya Everton ya English Premier League. Fabian Johnson atapewa fursa ya kuanza kama beki wa kulia wakati Matt Besler na Geoff Cameron wa Stoke wakianza kama mabeki wa katikati. Marcus Beasley, anayetarajia kucheza Kombe la Dunia kwa mara ya nne anapigiwa upatu kucheza kama beki wa kushoto.

Mlinda lango nambari moja wa Marekani Tim Howard
Mlinda lango nambari moja wa Marekani Tim HowardPicha: picture alliance/augenklick

Michael Bradley, mwanawe kocha wa zamani Bob Bradley, amepewa jukumu la kuwa kiungo. Bradely na Dempsey waliwavutia wachezaji wengine kujiunga na ligi ya Marekani, ambapo Bradely alihama Roma na kusajiliwa na Toronto baada ya Dempsey kuwashangaza wengi kwa kuhama Tottenham na kujiunga na Seattle.

Bradely amepangwa katika safu ya kiungo na Jermaine Jones, aliyehama Schalke na kujiunga na Besiktas. Wengine ni Graham Zusi wa Kansas City na Alejandro Bedoya wa Nates. Dempsey na Jozy Altidore wataongoza mashambulizi.

Njia pekee ya kufuzu katika awamu ya mwondowano ni kuwazaba Ghana na waombe Ujerumani ishinde mechi zake mbili za kwanza na ichezeshe wachezaji wasio na uzoefu katika mechi za mwisho za makundi.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Sekione Kitojo