1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jacob Zuma ateuliwa kiongozi mpya wa chama cha ANC

Josephat Charo19 Desemba 2007

Afrika Kusini itachukua mkondo gani

https://p.dw.com/p/CdkS
Kiongozi mpya wa chama cha ANC bwana Jacob Zuma akiangua kichekoPicha: AP

Chama tawala nchini Afrika Kusini, ANC, kimemchagua bwana Jacob Zuma kuwa rais wake mpya. Kwa mujibu wa matokeo ya kura iliyopigwa na wajumbe wa chama hicho, bwana Zuma amemshinda rais wa sasa wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki. Ushindi wa Zuma unampa nafasi nzuri ya kuweza kuwa rais wa Afrika Kusini katika uchaguzi utakaofanyika mwaka wa 2009.

Bwana Zuma mwenye umri wa miaka 65 anatazamwa na wengi kama mtu atakayetimiza mataumiani ya wengi nchini humo akilinganishwa na rais Mbeki ambaye ameelezwa kuwa mtu aliyejitenga na watu huku sera zake zikiwa za kiimla.

Enzi ya rais Thabo Mbeki imemalizika nchini Afrika Kusini na enzi ya bwana Jacob Zuma imeanza. Idadi kubwa ya wajumbe wa chama cha ANC walipitisha uamuzi huo kwenye mkutano wa chama hapo jana katika mji wa Polokwane. Rais Mbeki, atakayebakia madarakani kwa mwaka mmoja na nusu hadi uchaguzi mkuu ujao, alifanya kosa kubwa alipoondokana na misingi ya chama cha ANC na kutaka kudhibiti na kuidhinisha kila jambo.

Upinzani mkali dhidi ya rais Mbeki ulianza wakati alipomfuta kazi bwana Jacob Zuma kama makamu wa rais bila kukishauri chama cha ANC mnamo mwaka wa 2005 kwa madai ya kuhusika na ufisadi. Zuma alipata umaarufu mkubwa. Wafuasi wake wengi pamoja na watu wengine wengi ambao walikuwa hawaridhishwi na mfumo wa utawala wa rais Mbeki walimuunga mkono bwana Zuma.

Katika uchaguzi wa wajumbe katika mkutano wa chama na baadaye uchaguzi wa baraza kuu la chama cha ANC kumedhihirika mpasuko mkubwa wa kisiasa ndani ya chama huku chama kikigawanyika katika kambi mbili. Kambi inayomuunga mkono bwana Jacob Zuma na inayomuunga mkono rais Thabo Mbeki, viongozi wanaopingana, kugombana na bado wamo chamani kukipasua.

Mashirika yote nchini Afrika Kusini, na kunayo mashirika zaidi ya 4,000, yaliamua kumchagua mmoja kati ya Zuma na Mbeki na kuwatuma wajumbe wao kwenye mkutano wa mkoa na kazi ya kumteua mtu aliye ni chaguo lao.

Katika mikoa mitano mipya ya Afrika Kusini, iwe ni miongoni mwa vijana au wasichana, idadi ya wafuasi wa bwana Zuma iliongoezeka na kufikia takriban asilimia 60 nchini kote. Katika mkutano mkuu wa chama bwana Zuma alichaguliwa kwa asilimia 58,5 ya kura, ingawa ana sifa mbaya katika maswala ya fedha huku akielezewa kuwa mtu asiyetosheka na fedha alizonazo, huku akikabiliwa na kesi ya rushwa.

Na ingawa vyombo vya sheria vimepania kumhukumu, bwana Zuma bado anaonekana na wengi kuwa kiongozi anayefaa zaidi kuliko rais Mbeki ambaye ni msomi mwenye kuzingatia maadili na mtu anayejitenga na watu.

Bwana Zuma ana uwezo wa kuwafurahisha watu. Anazungumza lugha inayoeleweka, hucheza na kuimba wimbo aupendao sana unaoitwa ´Nipe silaha yangu´, wimbo wa wakati wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Na watu wengi huimba pamoja naye na kucheza na kushangilia.

Wana matumaini bwana Zuma atawafanyia mengi wale ambao mpaka leo hawajanufaika kutokana na maendeleo ya kiuchumi na bado wangali wanakabiliwa na umaskini uliokithiri. Idadi yao inakadiriwa kuwa nusu ya idadi ya wakaazi wote wa Afrika Kusini.

Wanatarajia pia bwana Zuma ataleta mfumo mpya wa uongozi utakaokuwa na midahalo ya wazi na uwezekano wa kuwepo upinzani. Bwana Zuma ameyaahidi yote haya, lakini pia ameziahidi kampuni kwamba hatabadili mkondo wa kiuchumi. Vipi atakavyoweza kuendeleza uchumi na kuhakikisha utoaji bora wa huduma za kijamii, ni kitendawili kinachosubiri jawabu.

Chama cha ANC chini ya utawala wa bwana Zuma kuanzia mwaka wa 2009 kitakuwa tofauti. Ikiwa kitakuwa kizuri zaidi, lazima kijionyeshe.