1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamhuri ya Afrika ya Kati yapata serikali

1 Aprili 2013

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Nicolas Tiangaye ametangaza baraza jipya la mawaziri baada ya kufanyika mapinduzi, ambalo asilimia wanatoka kwenye kundi la waasi la Seleka na chama cha zamani cha upinzani.

https://p.dw.com/p/187b6
Kiongozi mpya wa JAmhuri ya Afrika ya Kati, Michel Djotodia
Kiongozi mpya wa JAmhuri ya Afrika ya Kati, Michel DjotodiaPicha: Getty Images

Tiangaye, ambaye aliteuliwa kuwa waziri mkuu na kiongozi wa waasi, Michel Djotodia aliyeongoza mapinduzi na kujitangaza rais baada ya kuudhibiti mji mkuu wa Bangui, aliitangaza serikali hiyo mpya jana Jumapili jioni kupitia redio ya taifa. Mbali na kuwa rais, Djotodia amejiongezea nafasi ya waziri wa ulinzi.

Baraza hilo lenye mawaziri 34, linajumuisha tisa kutoka kundi la waasi wa Seleka, wanane wanatoka chama cha zamani cha upinzani na mmoja ni mshirika wa karibu wa rais aliyeondolewa madarakani, Francois Bozize, aliyelazimika kuikimbia nchi hiyo, baada ya waasi kuidhibiti Bangui. Mawaziri wengine 16 bado hawajulikani wanatoka makundi gani ya kiraia.

Nafasi muhimu zashikwa na Seleka

Nafasi za mawaziri wa petroli, usalama, maji na misitu, na mawasiliano, zimechukuliwa na waasi wa Seleka, ambapo wizara ya habari na mawasiliano ikiongozwa na Christophe Gazam Betty. Serikali hiyo mpya itakuwa madarakani kwa muda wa miaka mitatu, hadi hapo itakapoitisha uchaguzi mkuu ambao Bozize amepigwa marufuku kushiriki. Ijumaa iliyopita, Djotodia alitangaza kuongoza nchi kwa kuzingatia mkataba wa amani uliofikiwa mwezi Januari mwaka huu na ameahidi kuondoka madarakani mwaka 2016 na kwamba hatoshiriki katika uchaguzi.

Rais aliyepinduliwa, Francois Bozize
Rais aliyepinduliwa, Francois BozizePicha: AFP/Getty Images

Ufaransa na Marekani iliitaka serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kuheshimu mkataba wa kugawana madaraka uliosainiwa Gabon. Hata hivyo, Marekani imesema Waziri Mkuu, Nicolas Tiangaye, aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo kulingana na mkataba huo, ndiye kiongozi halali wa serikali.

Waasi wa Seleka walianza harakati za kuingia Bangui mwezi Desemba mwaka uliopita kabla ya kukubali kushiriki kwenye mazungumzo ya amani na serikali ya Rais Bozize. Baada ya siku kadhaa za kupora vitu na ghasia, wanajeshi waasi wameudhibiti mji wa Bangui kwa msaada wa kikosi cha Afrika katika ukanda huo.

Wanajeshi wengi waliouawa walikuwa watoto

Lakini taarifa za kushtua kuhusu watoto wanajeshi kuuawa katika mapambano ya kuudhibiti mji wa Bangui zimechapishwa na gazeti la Afrika Kusini jana Jumapili. Gazeti la Sunday Times limewanukuu wanajeshi wakisema kwamba wengi wa wanajeshi waasi waliouawa walikuwa ni watoto.

Mpiganaji mdogo wa Seleka
Mpiganaji mdogo wa SelekaPicha: AFP/Getty Images

Afrika Kusini imekataa kulizungumzia suala hilo. Afrika Kusini ina wanajeshi wake katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ikiwa ni kikosi cha kudhibiti usalama nchini humo kabla ya kuanguka kwa Bozize, jitihada ambazo zimeshindwa. Wanajeshi wake 13 waliuawa katika mapigano katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Wiki iliyopita, Umoja wa Afrika uliusimamisha uanachama Jamhuri ya Afrika ya Kati na imewawekea vikwazo waasi wa Seleka, akiwemo Djotodia. Tangu ijipatie uhuru wake kutoka Ufaransa, mwaka 1960, Jamhuri ya Afrika ya Kati imeshuhudia mapinduzi ya mara kadhaa. Wasiwasi wa kidini umeongezeka katika nchi hiyo yenye idadi kubwa ya Wakristo, tangu Djotodia ambaye ni Muislamu kujitangazia urais.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE,RTRE
Mhariri: Josephat Charo