1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamii ya kimataifa yataka azimio lenye mashiko kuhusu Syria

Admin.WagnerD16 Septemba 2013

Ufaransa,Uinegereza na Marekani zinataka azimio la uhakika na lenye mashiko kutoka umoja wa Mataifa kuihusu Syria jinsi itakavyosalimisha silaha zake za sumu kwa jamii ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/19i70
Picha: Reuters

Ufaransa inashinikiza kupitishwa kwa azimio lenye uzito kuongezea nguvu makubaliano yaliyoafikiwa mwishoni mwa juma kati ya Marekani na Urusi kuhusu Syria kukubali kuzisalimisha silaha zake za sumu kwa jumuiya ya kimataifa ili ziharibiwe.

Nchi hizo tatu zinataka kuwekwe muda maalum wa kuzisalimisha na kuziharibu silaha hizo za sumu za Syria.Makubaliano kati ya Marekani na Urusi yaliyoafikiwa siku mbili zilizopita, yanataka Syria kutangaza ina kiasi gani cha silaha hizo ifikapo mwishoni mwa wiki hii na kuzisalimisha ifikapo katikati ya mwaka ujao.Makubaliano hayo yataidhinishwa na azimio la umoja wa Mataifa.

Makubaliano hayo yameepusha kwa sasa shambulio kutoka Marekani na washirika wake dhidi ya utawala wa Rais wa Syria Bashar al Assad.Marekani na Ufaransa zimesema bado hatua za kijeshi ni jambo wanalolizingatia licha ya kusisitiza kuwa zingependelea suluhisho la kidiplomasia kutatua mzozo wa Syria.Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema nchi yake bado inalitafakari hilo.

Makubaliano ya kuzisalimisha silaha yasifiwa

Kerry amewasili mjini Paris leo kutoka Israel ambapo alinadi kuwa makubaliano aliyoyafikia na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov ndiyo fursa ya kuondoa silaha zote za sumu nchini Syria.Makubaliano hayo yamesifiwa kuwa hatua kubwa yenye mafanikio ya diplomasia zilizoendeshwa na Urusi.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei LavrovPicha: Reuters

Ufaransa ambayo haikushirikishwa katika mazungumzo hayo imesifu ufanisi huo lakini wakati huo huo kutilia mashaka utekelezwaji wake.Rais Hollande hapa jana aliyataja makubaliano hayo hatua muhimu lakini sio mwisho wa ufumbuzi wa mzozo wa Syria.

Ripoti kuhusu matumizi ya silaha kuwasilishwa rasmi

Hayo yanakuja huku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon akitarajiwa leo kuwasilisha rasmi ripoti kutoka kwa wachunguzi wa silaha za kemikali mjini Newyork kwa baraza la usalama la umoja huo.

Mkuu wa kundi la wachunguzi wa umoja wa Mataifa Ake Sellstrom akimkabidhi ripoti katibu mkuu wa umoja huo Ban ki Moon
Mkuu wa kundi la wachunguzi wa umoja wa Mataifa Ake Sellstrom akimkabidhi ripoti katibu mkuu wa umoja huo Ban ki MoonPicha: Reuters

Ban tayari ameshasema anatarajia ripoti hiyo kuthibitisha wazi kuwa silaha za sumu zilitumika katika shambulio la tarehe 21 mwezi uliopita karibu na mji wa Damascus ambapo mamia ya watu waliuawa.

Ushahidi wa aina gani ya sumu ilitumika katika shambulio hilo lililowaua watu 1,400 litatoa vidokezo ni upande gani wa vita vya Syria ulitumia silaha hiyo ya kemikali.

Mwandishi:Caro Robi/reuters/afp/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman