1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamii ya Mbilikimo wa DRC kusaidiwa kiuchumi

Tuma Provian Dandi23 Oktoba 2007

Baada ya kipindi kirefu cha kutotambuliwa kitaifa na kimataifa, jamii ya Mbilikimo inayoishi katika misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, huenda ikaanza kufikiriwa katika masuala mbalimbali

https://p.dw.com/p/C7rl
Maisha ya jamii ya Mbilikimo wa DRC yanavyoonekana
Maisha ya jamii ya Mbilikimo wa DRC yanavyoonekanaPicha: picture-alliance/dpa

Benki ya Dunia imeanza kufuatilia malalamiko yanayoeleza kwamba jamii ya Mbilikimo wanaoishi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-DRC, imepuuzwa kutokana na kutopewa mahitaji ya msingi anayopaswa kuwa nayo binadamu.

Kukumbukwa kwa jamii hiyo inayoishi katika misitu ya DRC inayosemeka kuwa ya pili kwa ukubwa duniani baada ya ile ya Amazon iliyoko Amerika ya Kusini, kunatokana na wao kuishi katika maeneo tajiri yenye kila aina ya maliasili.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Benki ya Dunia inaona kwamba watu wa jamii ya Mbilikimo wanaweza kupata faida kutokana na mazingira wanamoishi, ndiyo maana wameona umuhimu wa kuwekeza katika eneo la jamii hiyo.

Jamii hiyo inategemea neema za misitu ya Kongo kwa kupata chakula, malazi, dawa za asili kwa ajili ya afya na mapato yanayowasaidia kiuchumi.

Isitoshe jamii ya Mbilikimo inaitumia misitu ya Kongo kuwa ndiyo utambulisho wake.

Raia hao wanaofikia wastani wa Mbilikimo laki sita, wanachangia kiasi cha watu milioni 58 wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ambapo Wakongo milioni 40 wanasekana kuishi katika maeneo ya misitu minene.

Tayari Benki ya Dunia imekamilisha mpango wa kuwapeleka maofisa wake katika maeneo yanayokaliwa na watu wa jamii ya Mbilikimo huko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa lengo la kubuni na hatimaye kuanzisha miradi kadhaa.

Msemaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Bwana John Donaldson, amesema katika kipindi kifupi kijacho kutakuwa na mkutano mjini Kinshasa ambao taasisi hiyo kubwa ya fedha itawasilisha kile ilichokiandaa kuhusu mwenendo mzima wa maisha ya jamii ya Mbilikimo.

Ofisa huyo ameongeza kwa kueleza kwamba huo utakuwa mwanzo wa kuitambua jamii hiyo, pamoja na kupanua wigo kwa yale ambayo tayari yamepangwa kufanywa.

Baada ya jamii hiyo kuamka usingizini na kutaka kuzingatiwa kwa haki zao kama binadamu wengine, Benki ya Dunia imeridhia kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha kwamba miradi mingi inaanzishwa katika maeneo yao.

Kikubwa kichofikiriwa ni kuangalia namna gani jamii ya Mbilikimo inaweza kufaidi rasilimali za taifa kutokana na biashara ya mazao ya misitu hasa mbao na kilimo.

Kwa maana hiyo, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-DRC kwa kushirikiana na Benki ya Dunia itahakikisha kwamba maeneo yote yanayokaliwa na watu wa jamii hiyo yanakuwa na nyenzo bora za mawasiliano hasa barabara, pamoja na upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile shule, hospitali, na kadhalika.

Mmoja wa wasemaji kutoka jamii ya Mbilikimo katika eneo la Bukavu Bwana Adrian Sinafasi, amesema lengo lao ni kuitaka Benki ya Dunia kuwashirikisha katika mambo yote yatakayowezesha kupatikana maendeleo ya kiuchumi.

Bwana Sinafasi amesema mazao ya msituni kama asali, mbao, wanyama pori, uyoga na mitishamba ni suluhisho la maendeleo kwa jamii ya Mbilikimo.