1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Janga la ukame Mashariki mwa Afrika Magazetini

Oumilkheir Hamidou
7 Aprili 2017

Balaa la ukame, kitisho cha wimbi kubwa zaidi la wakimbizi na jinsi serikali kuu ya Ujerumani inavyopania kusaidia juhudi za kukabiliana na vyanzo vya ukimbizi ni miongoni mwa mada za Afrika magazetini wiki hii

https://p.dw.com/p/2arcf
Äthiopien Bundesentwicklungsminister Gerd Müller in der Somali-Region
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Tunaanzia na janga la ukame na jinsi linavyoathiri maeneo ya mashariki mwa Afrika. Gazeti la Berliner Zeitung limezungumzia ziara ya waziri wa misaada ya maendeleo Gerd Müller aliyewazuru wahanga wa janga la ukame linalopiga nchini Ethiopia ambako mvua hazijanyesha tangu juni mwaka jana. Berliner Zeitung linazungumzia kisa cha Amren Mualin, bibi wa miaka 42 aliyelazimika kuyapa kisogo maskani yake pamoja na wanawe 7 kati ya 13 na kukimbilia katika kituo kinachosimamiwa na mashirika ya misaada ya kiutu kusini mashariki mwa Ethiopia. Mumewe na watoto wake waliosalia wamebakia na mifugo iliyokondeana. Mbuzi na kondoo wao kati ya 350 na 400 wamekufa kutokana na ukame.

Balaa la ukame halina dalili ya kumalizika

Waziri wa misaada ya maendeleo Gerd Müller linaandika gazeti la Berliner Zeitung amelitembelea eneo hilo jumatatu na jumanne iliyopita ili kujionea mwenyewe hali halisi namna ilivyo. Gerd Müller ameahidi wizara yake itazidisha kwa Euro milioni 100 misaada yake na kufikia Euro milioni 300. Sehemu kubwa itakabidhiwa shirika la Umoja wa mataifa linaalowahudumia watoto UNICEF. Ukame mbaya kabisa kuwa kulikumba eneo la Mashariki mwa Afrika tangu miaka 30 iliyopita unawaathiri watu wasiopoungua milioni 22 pamoja na mifugo yao na mazao yao ya kilimo. Yanaoathirika zaidi ni maeneo ya Sudan Kusini, Somalia , Ethiopia na Kenya.

Balaa la ukame katika eneo la mashariki mwa Afrika limechambuliwa pia na gazeti la mjini Cologne, Kölner Stadt Anzeiger linasema asili mia 80 hadi 90 ya mifugo wamekondeana na kufa  kwa ukame nchini Ethiopia. Gazeti linasema hata kama mvua itanyesha mwezi huu wa Aprili, patahitajika miezi kadhaa hadi majani yatakapoanza kuota.

Gerd Müller awasilisha mbele ya Umoja wa Afrika mpango wake wa Marshallplan

Berliner Zeitung limezungumzia pia jinsi waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu Gerd Müller alivyowasilisha mpango wake wa kuinua maendeleo barani Afrika-Marshal plan, mbele ya halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Abeba mapema wiki hii. Kwesi Quartey, naibu mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika ameutaja mpango wa waziri Gerd Müller kuwa ni jibu la kuongezeka wahamiaji kinyume na sheria barani Ulaya. Berliner Zeitung limemaliza kwa kukumbusha kwamba mpango  huo  wa Marshal uliochapishwa january iliyopita unazungumzia juhudi za kuimarisha miradi ya elimu, biashara na uwekezaji.

Wakimbizi wengi wanatokea Afrika

Mzozo wa wakimbizi umezungumziwa pia na mhariri wa gazeti la Der Tagesspiegel linalosema serikali kuu ya Ujerumani imepania kukabiliana na chanzo cha mzozo huo. Gazeti linasema idadi ya wakimbizi wanaoingia Ulaya kutoka Afrika inaongezeka mno. Mnamo miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu idadi hiyo imeongezeka kwa asili mia 51 ikilinganishwa na idadi ya wakimbizi kama hao kutoka Afrika walioingia mwaka mmoja uliopita katika nchi za Umoja wa ulaya. Idadi hiyo imechapishwa na shirika la uhamaji IOM. Wakimbizi wa Afrika linaandika gazeti la der Tagesspiegel wanapitia Misri na Libya. Huko kuna makundi ya wahalifu wanaowasafirisha wakimbizi hao kupitia bahari ya kati hadi Italia.Takriban wakimbizi wote walioingia katika nchi za Umoja wa ulaya miezi mitatu iliyopita wanatokea Afrika, na wengi wao ni vijana wanaokimbia sio tu vita vya wenyewe kwa wenyewe na machafuko ya kisiasa, bali hasa umaskini na ufisadi. Der Tagesspiegel linazitaja Senegal, Nigeria, Guinea Gambia na Côte d'Ivoire kuwa nchi wanakotokea wakimbizi wengi zaidi.

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/PRESSE

Mhariri: Gakuba, Daniel