1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa madeni ya Ugiriki

4 Mei 2015

Janga la wakimbizi katika bahari ya Mediterenia,rais wa Ujerumani na mgogoro wa madeni ya Ugiriki na kashfa ya upelelezi ya idara ya ujasusi ya Ujerumani BND ni miongoni mwa mada zilizohanikiza magazetini.

https://p.dw.com/p/1FJge
WakimbiziPicha: Reuters/Marina Militare

Tunaanzia katika bahari ya Mediterenia ambako kila kukicha ripoti za kuhuzunisha zinagonga vichwa vya habari kuhusu mikururo ya wakimbizi wanaoyatia hatarini maisha yao ili kusaka amani na maisha bora barani Ulaya.Gazeti la "Emder Zeitung" linaandika:"Balaa halina mwisho":Kwa mara nyengine tena wakimbizi kadhaa kutoka Afrika Kaskazini wameokolewa katika bahari ya Mediterenia.Kwa mwisho wa wiki hii tuu idadi yao inasemekana kufikia watu 4500.Watu walioyapa kisogo maskani yao kwa matumaini ya kujipatia maisha bora barani Ulaya.Katika mataifa yale yale ambako haki za binaadam ni adhimu,hali hii inawafanya watu wasijue la kufanya.Umaskini,vita na kuandamwa kisiasa ndio sababu kwanini watu wengi wanajikuta hawana njia nyengine isipokuwa moja tu:kuihama nchi yao.Umoja wa Ulaya-Ujerumani na Ufaransa zikikamata mstari wa mbele- unabidi uwajibike.Uwajibike kwa namna mbili:Pamoja na washirika wao,wasaidie kupunguza vita na vitisho ili maisha yarejee kuwa ya kawaida katika nchi husika,na wakati huo huo kuwafungulia milango wenye shida wanaotutaka tuwasaidie.

Rais Gauck na madai ya fidia ya Ugiriki

Mada nyengine iliyogonga vichwa vya habari magazetini hii leo ni kauli ya rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck kuhusu mgogoro wa madeni ya Ugiriki na madai yake ya kutaka ilipwe fidia na Ujerumani.Gazeti la "Baldische Neueste Nachrichten" linahisi rais amebadilisha msimamo wake kuhusu suala hilo.Gazeti linaendelea kuandika:"Ni mabidiliko makubwa ya maoni ya rais wa shirikisho Joachim Gauck haya-na ni jambo geni pia.Mwaka kama mmoja uliopita,alipokuwa ziarani nchini Ugiriki,rais wa shirikisho alijibu miito ya kulipwa fidia kwa maovu waliyotendewa wagiriki wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia kwa kusema utaraatibu wa kisheria umeshakamilishwa.Hivi sasa lakini anatatanisha anapozungumzia kuhusu "uwezekano wa kulipwa fidia"na kuwapa kichwa wale ambao wanachokitafuta zaidi sio makosa yaliyofanywa na Ujerumani wakati ule bali uwezo wao wa kisiasa.

Kashfa ya upelelezi

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu kashfa ya upelelezi inayolihusu shirika la upelelezi la Ujerumani BND.Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linaandika:"Kansela Angela Merkel atalazimika kujieleza.Kupelelezana kati ya marafiki,hilo haliwezekani kamwe-aliwahi kusema wakati mmoja.Kipeo cha kashfa hii ambapo yadhihirika bara lote la Ulaya lilimulikwa na shirika la ujasusi la Marekani NSA ni cha juu.Kupelelezana kati ya marafiki ni jambo linalowezeklana tena sana!Kisichowezekana kwa sasa ni hali ya kutosema chochote kansela.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlanmdspresse

Mhariri: Gakuba Daniel