1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jaribio la kombora la Korea Kaskazini lashindwa

Isaac Gamba
22 Machi 2017

Kombora la Korea Kaskazini linaonyesha limeripuka muda mfupi baada ya kufyetuliwa hii leo tarehe (22.03.2017).Wanajeshi wa Marekani na Korea ya Kusini wamesema baada ya kuchunguza idadi kadhaa ya majaribio ya makombora.

https://p.dw.com/p/2Zkjl
Kim Jong-Un
Picha: picture-alliance/AP Photo/W. Maye-E

Jaribio hilo la kombora limefanyika kutoka katika mji wa karibu wa Wonsan ulioko upande wa pwani mashariki mwa Korea Kaskazini ikiwa ni sehemu ile ile ambayo nchi hiyo mwaka jana ilifyatua makombora  kadhaa ya masafa ya kati ambapo moja kati ya makombora hayo lilishindwa.

Msemaji wa vikosi vya Marekani katika ukanda wa Pasifiki Dave Benham amethibitisha kushindwa kwa kombora hilo mara tu baada ya kufyatuliwa na kuongeza kuwa kombora hilo limeripuka sekunde chache baada ya kurushwa.  Haikuweza kufahamika mara moja ni kombora la aina gani lililorushwa  na Korea Kusini ilikuwa ikifuatilia suala hilo kwa ajili ya kutoa taarifa zaidi.

Kuongezeka kwa idadi ya majaribio ya makombora kumeibua hali ya tahadhari kuhusiana na jinsi gani ulimwengu unaweza kukabiliana na hatua hiyo ya Korea Kaskazini.

Korea kaskazini ilirusha makombora manne ya masafa marefu kutoka eneo la jirani na upande wa pwani magharibi mwa nchi hiyo mnamo Machi 6, na pia wiki hii ilifanya jaribio la kombora la kinyuklia huku kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong Un akisema  hatua hiyo imefungua ukurasa mpya katika mchakato wake wa kutengeneza silaha za nyuklia.

Hatua hii inakuja baada ya mjumbe maalumu wa Marekani kuhusiana na sera za Korea Kaskazini, Joseph Yun kukutana na mwenzake  wa Korea Kusini mjini Seul kujadili jinsi ya kukabiliana dhidi ya hatua zinazohusiana na mpango wa silaha kali wa Korea Kaskazini.

 

Marekani yajadili jinsi ya kukabiliana na uchokozi wa Korea Kaskazini

Deutschland G 20 Außenministertreffen in Bonn - Rex Tillerson
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Rex TilersonPicha: picture alliance/dpa/B. Smialowski

Wiki iliyopita Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson alizuru Japan, Korea Kusini na China na suala linalohusiana na jinsi gani wanaweza kukabiliana na hatua hiyo ya Korea Kaskazini lilikuwa ni suala kubwa katika mazungumzo yake.

Tilerson alisema sera inayohusiana na uvumilivu juu hatua hizo za majaribio ya makombora zinazofanywa na Korea Kaskazini sasa umefikia mwisho, na kuwa mjadala juu ya kuchukua hatua nyingine dhidi ya taifa hilo ikiwa ni pamoja na hatua za kijeshi hivi sasa uko mezani  iwapo Korea Kaskazini itafanya vitendo vya uchukozi dhidi ya Marekani au Korea Kusini.

Korea Kaskazini imefanya majaribio mawili  ya makombora ya nyukilia pamoja na majaribio ya makombora kadhaa tangu mwanzoni mwa mwaka jana ikikaidi azimio la Umoja wa Mataifa na inaaminika kuwa iko katika mchakato wa kutengeneza silaha za nyukilia ambazo zinaweza kuizuru Marekani.

Mwandishi: Isaac Gamba/ rtre

Mhariri  :  Mohammed Abdul-Rahman