1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jaribio la mapinduzi Sudan Kusini

Mohamed Abdulrahman16 Desemba 2013

Rais Salva Kirr asema amelishinda jaribio la kutaka kumpindua, akimshutumu hasimu yake Riek Machar kuhusika na njama hiyo .

https://p.dw.com/p/1AaUH
Rais wa Sudan kusini- Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: Reuters

Taarifa zinasema mapigano yalizuka katika kambi za kijeshi karibu na eneo la kati la mji mkuu, Juba, kabla ya usiku wa manane wa kuamkia Jumatatu na kuzagaa kote mjini humo. Maafisa wa kibalozi na raia walioshuhudia wamesema kulisikika milio mikubwa ya risasi na mizinga.

Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya raia 800 walioingiwa na hofu walikimbilia kutafuta hifadhi katika kituo cha Umoja huo karibu na uwanja wa ndege, wengi wakiwa wanawake na watoto. Miongoni mwao ni majeruhi saba akiwemo mtoto wa miaka miwili, huku wakaazi wengi wakijifungia majumbani mwao.

Hali yadhibitiwa

Rais Salva Kirr amesema mapigano hayo lilikuwa jaribio la mapinduzi na kumlaumu hasimu yake, makamu wa zamani wa rais Riek Machar ambaye alifukuzwa kazi mwezi Julai.

Salva Kirr alitamka katika taarifa yake kwa taifa "serikali yenu imeidhibiti kikamilifu hali ya usalama mjini Juba, washambuliaji wamekimbia na majeshi yenu yanawasaka. Nawaahidi sheria itachukua mkondo wake."

Kiongozi huyo alisema hatoruhusu tena jambo kama hilo kutokea katika taifa hilo jipya na analaani kitendo hicho alichokiita cha uhalifu mkubwa.

Amri ya kutotoka nje imetangazwa kuanzia saa 12 za magharibi leo hadi 12 za asubuhi kesho Jumanne.

Msemaji wa jeshi, Phil Aguer, alisema kwa njia ya redio mjini Juba kwamba wanajeshi watiifu kwa Rais Kirr wanaidhibiti hali ya mambo, huku maafisa wakisema kwamba kuna watu waliokamatwa, lakini hatima ya Machar haijulikani. Pia hakukuwa na maelezo yoyote kuhusu waliouawa au kujeruhiwa katika mapigano hayo.

Machar analiongoza kundi la upinzani ndani ya chama tawala SPLM na anaonekana kuwa mpinzani mkubwa wa Kirr.

Wasi wasi na mivutano ya kisiasa ilizidi kuwa mikubwa wiki za hivi karibuni na mapema mwezi huu viongozi kadhaa wa ngazi ya juu wa SPLM akiwemo Machar na Rebeca Garang, mjane wa kiongozi wa zamani wa Sudan ya Kusini, John Garang, walimpinga Rais Kirr hadharani, wakimshutumu kuwa ni dikteta.

Hatua za ziada zachukuliwa

Balozi za Uingereza na Marekani mjini Juba, zimewataka raia wao kujiepusha na nyendo zisizo za lazima. Afisa mmoja wa kibalozi amesema wanajeshi watiifu kwa rais wamewekwa katika vituo vyote muhimu. Maafisa wa shughuli za usafiri wa ndege wanasema uwanja wa ndege wa Juba umefungwa kwa muda usiojulikana sawa na mipaka yote na nchi jirani za Uganda na Kenya.

Umoja wa Mataifa umesema una wasiwasi mkubwa kuhusu mapigano hayo na kwamba unawasiliana na uongozi nchini humo. Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, Bibi Hilde Johnson, amezitaka pande zote kusimamisha mapigano na kuwa na uvumilivu.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/AFP/AP
Mhariri: Mohamed Khelef