1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jasusi wa Libya apokewa kishujaa nyumbani

Aboubakary Jumaa Liongo21 Agosti 2009

Jasusi wa zamani wa Libya anayetuhumiwa kwa ulipuaji wa ndege ya Marekani huko Lockerbie miaka 11 iliyopita, Abdel Baset al-Megrahi amepata mapokezi makubwa aliporejea mjini Tripoli kufuatia msamaha wa huruma aliyopata

https://p.dw.com/p/JFkb
Jasusi wa zamani wa Libya Abdel Basset Ali al-MegrahiPicha: AP

Hata hivyo Uingereza imeelezea kusikitishwa kwake na mapokezi hayo aliyopewa Mengrah ambaye anaumwa kansa ya kibofu cha mkojo iliyofikia katika hatua mbaya

Maelfu ya vijana wakiongozwa na mtoto wa kiongozi wa Libya Saif al-Islam Gadaffi  walijazana katika uwanja wa ndege mjini Tripoli jana usiku kumlaki jasusi huyo wa zamani wa Libya anayetuhumiwa kwa kuhusika na kuilipua ndege ya Pan Am ambapo watu 270 waliuawa.

Akiwa amevalia suti nyeusi na fimbo al Megrahi alionekana mchovu wakati alipojitokeza nje ya ndege iliyomrejesha na kupokewa na mtoto huyo wa Kanali Gadaffi aliyevalia nguo nyeupe za kiasili , ambapo watu waliyofuruka walimtupia maua.Kwa mujibu wa madaktari kansa hiyo ya kibofu cha mkojo imefikia kiwango kikubwa na kwamba ana muda mfupi wa kuishi.

Mtoto huyo wa Gadaffi  mwaka jana aliahidi kufanya kila njia kumrejesha jasusi huyo nyumbani, na wakati alipompokea alinyanyua ngumi juu kuashiria ushindi, kabla ya kuchukuliwa katika msafara wa magari meupe ya kifahari.

Vipaza sauti vilipiga nyimbo za kizalendo, huku watu waliyojitokeza wakipeperusha bendera za Libya na Scotland.

Labour Parteitag in Manchester David Miliband
Waziri wa Nje wa Uingereza David MilibandPicha: AP

Hata hivyo mapokezi hayo ya kishujaa aliyoyapata al Megrahi yameisikitisha serikali ya Uingereza, ambapo Waziri wa Mambo ya wa nchi hiyo David Miliband amesema hakukuwa na shinikizo lolote kwa serikali ya Scotland kutoka serikali kuu ya Uingereza kutaka kuachiwa kwa jasusi huyo.

Waziri huyo wa nje wa Uingereza amesema kuwa ni udhalilishaji kusema kuwa al Megrahi ameachiwa kwa misingi ya kutaka kuimarisha uhusiano na Libya ikiwa pia ni pamoja na kufungua milango zaidi kwa makampuni ya mafuta ya Uingereza nchini Libya.

Waziri Miliband amesema kuwa uamuzi wa kuachiwa kwa al Megrahi umefanyika kwa kufuata misingi ya katiba ya Scotland na kwamba hakukuwa na mbinyo wowote kutoka London.

Ameongezea kuwa ameiambia serikali ya Libya jinsi itakavyoshughulika na jasusi huyo baada ya kurejeshwa ndilo jambo muhimu linalosubiriwa.

Kwa upande wake Rais Barck Obama wa Marekanli alitaka jasusi huyo kupewa kifungo cha nyumbani na si kuwa huru.

Obama äußert sich zur Freilassung der Journalistinnen Euna Lee und Laura Ling
Rais Barack ObamaPicha: picture alliance/dpa

´´Tunawasiliana na serilkali ya libya ili kuhakikisha ya kuwa mtu huyu si anakaribishwa nyumbani kwake bali anakaribishwa kwenye kifungo cha nyumbani.´´

Mapema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton ambaye jimbo lake la New York ambalo miongoni mwa vijana waliyouawa katika shambulizi hilo la Lockerbie, wengi walitokea huko alielezea kusikitishwa kwake na kuachiwa kwa jasusi huyo.

Ndugu wa watu waliyokufa katika shambulizi hilo nao pia wameelezea kusitikishwa kwao na kuachiwa huru kwa al -Megrahi.

Susan Cohen,ambaye binti yake Theodora ni miongoni mwa waliyouawa amesema uamuzi uliyotolewa na Sctoland ni wa kutisha.

Al Megrahi ambaye aliendelea kudai kutohusika kwake, alihukumiwa kifungo cha maisha na mahakama yaUholanzi, chini ya sheria za Scotland, mwaka 2001.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters/AFP

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman