1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, benki zimepata funzo lo lote?

15 Septemba 2010

Mgogoro wa fedha duniani ulifikia kipeo chake, benki ya uwekezaji ya Marekani Lehmann Brothers ilipokwenda muflis Septemba 15 mwaka 2008.

https://p.dw.com/p/PCXq
Pedestrians walk pass Lehman Brothers headquarters on Wednesday, June 10, 2008, in New York. Lehman Brothers Holdings Inc., the nation's fourth-largest investment bank whose shares have fallen more than 80 percent this year as investors lost confidence amid mounting losses also said Wednesday it lost $3.9 billion during the third quarter due to wrong-way bets on mortgage securities and other risky assets. (AP Photo/Jin Lee
Makao makuu ya zamani ya Lehmann Brothers mjini New York.Picha: AP

Serikali katika nchi mbali mbali zilitumia Euro bilioni 15 katika jitahada za kupunguza athari za mgogoro huo katika sekta ya uchumi.Tangu wakati huo viongozi na wanasayansi wanajaribu kuwa na mfumo mpya wa fedha duniani. Je, jitahada hizo zimefanikiwa kwa umbali gani? Benki nazo zimejifunza cho chote ?

Professor Dr. Udo Steffens, Vorsitzender der Geschäftsführung und Präsident der Frankfurt School of Finance & Management
Rais wa Chuo Kikuu cha Uchumi na Uongozi cha Frankfurt, Profesa Dr. Udo Steffens.Picha: Frankfurt School of Finance & Management

Rais wa chuo kikuu cha uchumi na uongozi mjini Frankfurt, Profesa Udo Steffens, anasema benki zimejifunza kutokana na mzozo wa fedha na uchumi uliotokea duniani.

"Bila shaka benki zimepata funzo. Hata ikiwa walichojifunza hasa kinahusika na uongozi wa ndani, mikakati na mifumo ya bidhaa zake."

Akifafanua zaidi,Profesa huyo wa uchumi anasema, kanuni za kurekebisha mfumo wa benki na taasisi za fedha nchini Ujerumani na hata kwengineko ulimwenguni ndio kwanza zitaanza kufanya kazi kisheria.

Ujerumani ilikuwa nchi pekee kupiga marufuku biashara ya walanguzi katika masoko ya fedha, lakini hiyo haikusaidia kwani benki zingine za kimataifa ziliweza kuhamisha biashara hiyo ya ulanguzi kwengineko. Mnamo mwezi wa Agosti, serikali ya Ujerumani vile vile ilipitisha sheria ya kufanywa mageuzi katika mfumo wa benki. Kuanzia mwaka 2011, benki zinatakiwa kuweka kando akiba maalum,ili walipakodi wasijekupachikwa tena mzigo wa kuziokoa benki, iwapo mgogoro mwengine utazuka.

Kwa upande mwingine, katika kanda ya Ulaya hivi karibuni kumepitishwa uamuzi muhimu kabisa tangu ulipotokea mgogoro wa fedha duniani. Kuambatana na kanuni hiyo mpya, kuanzia mwaka 2011 kutakuwepo idara mpya tatu kusimamia shughuli za benki,mashirika ya bima na masoko ya hisa. Wasimamizi hao watakuwa na usemi wa mwisho, taasisi za fedha zitakapojikuta katika matatizo. Lengo ni kuepukana na mgogoro mwingine wa fedha.

Kwa maoni ya mwanauchumi Max Otte, misingi ya kurekebisha masoko ya fedha ni rahisi. Kwanza kabisa ni mtaji wa benki. Akitoa mfano anasema, benki kubwa kabisa ya Ujerumani "Deutsche Bank" huendesha shughuli zake kwa kutumia asilimia 1.5 ya mtaji wake. Lakini benki zikilazimishwa kutumia kati ya asilimia 8 au 9 ya mtaji wake, hiyo humaanisha kuwa walanguzi watatumia sehemu kubwa zaidi ya fedha zao wenyewe. Kwa hivyo watakuwa makini zaidi. Anasema katika ulimwengu wa kibepari mtaji ni muhimu kabisa.

Itakumbukwa kuwa benki ya Lehmann Brothers wakati ilipofilisika, sehemu ya mtaji wake katika biashara ya dola bilioni 500 ilikuwa dola bilioni 20. Jumapili iliyopita,baraza la wasimamizi wa benki na viongozi wa benki kuu kutoka nchi 27 walikubaliana kuwa na sheria kali zaidi. Yaani baada ya miaka sita ijayo, benki zitapaswa kuweka asilimia 7 ya mtaji wake kwa ajili ya biashara ya hisa na malipo ya riba.Lakini mwanauchumi Steffens anasema:

"Marekebisho hayo yatabakia kwenye karatasi tu. Kwani masoko ya fedha hayatokubali kuwekewa vizingiti. Badala yake benki hizo mara kwa mara zitatafuta njia ya kupata uvumbuzi mpya."

Professa huyo wa uchumi anauliza: "Je, masoko ya fedha na wahusika wake waachiliwe kusababisha mizozo kwa kiwango kama kile kilichoshuhudiwa?"

Mwandishi:Zhangh,Danhong/ZPR/P.Martin

Mpitiaji:M.Abdul-Rahman