1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, huu ndio mwisho wa ugaidi?

2 Mei 2011

Mtu aliyeaminika kuwa gaidi nambari moja duniani, Osama bin Laden, ameuawa kwa ushirikiano wa vikosi vya Marekani na Pakistan. Hapana shaka hii ni hatua kubwa, lakini kama huu si mwisho wa Al Qaeda.

https://p.dw.com/p/117Yq
Osama bin Laden
Osama bin LadenPicha: AP

Takribani kwa miaka kumi kamili, Marekani na ulimwengu wa kimagharibi ulikuwa ukisubiri habari hii: Osama bin Laden amekufa. Lakini kiongozi huyu wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda akabakia hai, na hivyo kuzidisha moto kwenye vikosi maalum vya Marekani, kama alivyoahidi aliyekuwa Rais wa taifa hilo wakati wa mashambulizi ya Septemba 11, mwaka 2001, George W. Bush. Hapana shaka, habari hii iliyokuja sasa inashangiriwa kama ushindi mkubwa kwa upande wa Marekani.

Sio kwamba si sahihi: Bin Laden hakuwa na dhamana tu ya vifo vya watu 3,000 kutokana na mashambulizi hayo ya Septemba 2001. Bali wakati wote wa maisha yake alikuwa ni alama na kiunganishi cha mtandao wa kigaidi duniani, ambayo imethubutu kuendesha mashambulizi yenye umwagaji damu mkubwa.

Bin Laden alikuwa ni kama fumbo, ambalo kuwepo kwake kulikuwa kunawashajiisha vijana wa makundi ya kigaidi, na ambalo pia lilinyima usingizi taifa kubwa la Marekani kwa takribani muongo mzima.

Wamarekani wakishangiria kifo cha Osama bin Laden
Wamarekani wakishangiria kifo cha Osama bin LadenPicha: AP

Fumbo hili sasa limefumbuliwa. Mtandao wa kigaidi umepoteza kichwa chake. Vikufu vya mnyororo wake vimetenguliwa na ule mshikamano wake, angalau kwa sasa, umedhoofishwa. Kwa mauaji haya, hatimaye Marekani imeweza kujikosha na aibu ya Septemba 11. Mpaka hapo, hali ni nzuri.

Hata hivyo, bado kumebakia maswali mengi ya kujibiwa. Kwa mfano, iliwezekanaje kwamba Bin Laden alikuwa amejificha katikati ya ardhi ya Pakistan, katika sehemu ambayo si mbali sana na mji mkuu wa Islamabad, kwa kipindi chote hicho bila kuonekana? Je, daima operesheni ya Marekani kumtafuta ilisaidiwa na Pakistan?

Na bado kuna mengine: Vipi kuhusu mtu namba mbili kwenye mtandao wa Al Qaeda, Ayman Al Zawahiri, ambaye bado anaaminika kujificha kati ya mpaka wa Pakistan na Afghanistan? Kwa namna gani mitandao mingine ya kigaidi iliyozagaa ulimwenguni inajitegemea, mbali na Al Qaeda?

Msomaji gazeti nchini Japan akisoma taarifa ya kifo cha Osama bin Laden
Msomaji gazeti nchini Japan akisoma taarifa ya kifo cha Osama bin LadenPicha: AP

Inahofiwa kuwa, kwa siku zijazo wafuasi wa Al Qaeda watajipanga tena kuendeleza lengo na dhamira yao. Mashambulizi ya karibuni huko Marrakesh, Morocco, na kuwepo kwa vitisho vya mashambulizi ya Al Qaeda nchini Ujerumani, kuna maana kwamba bado kazi ingalipo. Na kwamba hata baada ya miaka 10 tangu mashambulizi ya Septemba 11, si ugaidi wala vitisho vyake vilivyoweza kutokomezwa.

Hata wimbi la mabadiliko linalotokea hivi sasa katika ulimwengu wa Kiarabu, linaweza kuibua sura mpya kabisa ya jihadi. Maana kama vurugu na mapinduzi kwenye eneo hili hazikusababisha uhuru na utulivu wa kweli, basi itakuwa rahisi kufungua milango kwa ugaidi.

Itakuwa kituko kuamini kuwa kifo cha Osama Bin Laden ndio mwisho wa ugaidi duniani. Bin Laden ameondoshwa tu kama kiongozi wa mtandao wa kigaidi. Lakini mtandao wake bado utaendelea na dhamira yake, maana ile misingi ya ugaidi haiwezi tu kufa nguvu za kijeshi pekee, bali pia na za kisiasa. Ingawa kifo chake kinaweza kuwa hatua kubwa katika vita dhidi ya ugaidi duniani, bado safari ya kufikia amani ya kweli tunayo.

Mwandishi: Daniel Scheschkewitz/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo