1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Je, waziri ameharibika kichwa?"

Maja Dreyer10 Julai 2007

Vita vya Iraq, juhudi za kutafuta amani kati ya Israel na Wapalestina pamoja na mapendekezo ya waziri wa ndani wa Ujerumani kuweka sheria kali zaidi dhidi ya magaidi – hizo ndizo mada zinazozingatiwa leo.

https://p.dw.com/p/CHSS

Kwanza ni uchambuzi wa mhariri wa “Nordwest-Zeitung” juu ya hali nchini Iraq:

“Hakuna shaka kwamba siku hizi itambidi rais Bush wa Marekani kuamua aelekee wapi katika sera zake za Iraq. Hata ikiwa anakataa kubadilisha sera hizo, hali halisi inamlazimisha kufanya hivyo katika wiki au miezi ijayo, kwani Marekani inashindwa katika vita vya Iraq. Malengo yaliyowekwa hayawezi kufikiwa. Bush hana vyombo wala busara kuweza kuleta amani na usalama Iraq. Kwa hivyo kuna njia moja tu, yaani kuondoka kutoka huko.”

Ni gazeti la “Nordwest-Zeitung”. Mhariri wa “Tageszeitung” la mjini Berlin anachambua ziara ya Umoja wa nchi za Kiarabu ambayo inatarajiwa kufanywa nchini Israel wiki hii. Akitambua kwamba matarajio ni madogo baada ya Hamas kutawala eneo la ukanda wa Gaza, mhariri huyu anasisitiza kuwa hasa wakati wa vita kati ya Wapalestina lazima kuwa na msimamo wa pamoja upande wa kimataifa. Ameandika:

“Kundi la Hamas liko imara. Halikubali kushindwa siyo kwa vikwazo vya nchi za Magharibi wala kwa nchi muhimu za kiarabu ambazo zimejaribu kupatanisha katika mzozo huu kati ya Wapalestina. Hamas haiwezi kushawishiwa si kwa fedha wala kwa shinikizo. Hata hivyo, wale ndani ya Hamas ambao hawana msimamo mkali sana wanataka kuzungumza na nchi za Magharibi. Kuachiliwa huru kwa mwandishi wa BBC Alan Johnston, ilikuwa kama ishara. Ikiwa watu hao wa Hamas wanakataliwa mazungumzo, faida ni kwenye upande wa mrengo wa siasa kali wa Hamas. Pia kukataa mazungumzo na Hamas kunamaanisha kuharibu majaribio yote ya kupata amani na jamii ya Wapalestina iliyoichagua Hamas katika uchaguzi wa kidemokrasi.”

Hapa nchini Ujerumani, mjadala juu ya mapendekezo ya waziri wa ndani, Wolfgang Schäuble, ya kuweka sheria kali zaidi kuzuia mashambulio ya kigaidi, unaendelea.

“Je, ameharibika kichwa?”

Hivyo ndivyo anavyouliza mhariri wa “Kölnische Rundschau” kama kichwa cha uchambuzi juu ya mapendekezo haya ya waziri Schäuble. Na anaendelea kuandika:

“Waziri huyu anataka watuhumiwa wa mashambulizi ya kigaidi waangamizwe ikiwa inahitajika na wengine ambao wanaaminika kuwa hatari kwa jamii wawekwe gerezani, vilevile anataka kuwapiga marufuku wale Waislamu wenye msimamo mkali kutumia simu ya mkononi na pia mtandao wa Internet. Ikiwa mapendekezo haya yatatekelezwa, sura ya Ujerumani ingebadilika sana. Taifa hili huru la kisheria ambalo msingi wake ni kuamini watu hawana kosa na hukumu zitegemee uzito wa uhalifu, basi mfumo huu ungeathirika sana.”

Na hatimaye juu ya suala hili ni gazeti la “Die Welt”:

“Waziri wa ndani anataka kuwaonya wananchi ambao kwa maoni yake hawatambui hali halisi, wafahamu hatari za ugaidi wa kimataifa ni kubwa. Ndiyo sababu anarudia ujumbe wake kwamba Ujerumani pia inalengwa na magaidi wa Kiislamu, mashambulio yanaweza kutokea na serikali inahitaji kuwa na vyombo vya kuwalinda raia. Ni sawa tu kuwa waziri Schäuble anajaribu kupunguza hatari. Lakini badala ya kuharibu uhuru wa wananchi kwa kuweka sheria kali anapaswa kutambua kuwa hatari haiwezi kuondoshwa kabisa.”