1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jean Todt apata mpinzani urais wa FIA

2 Septemba 2013

Jean Todt, rais wa shirika linaloongoza mchezo wa mbio za magari duniani FIA, atakabiliwa na upinzani kwa urais wake mwezi Desemba, baada ya David Ward kutangaza kugombea nafasi hiyo.

https://p.dw.com/p/19aOB
FIA President Jean Todt speaks after a meeting with the Brazil's President Dilma Rousseff at the Planalto Palace August 23, 2012. REUTERS/Ueslei Marcelino (BRAZIL - Tags: SPORT MOTORSPORT POLITICS F1)
FIA Präsident Jean TodtPicha: Reuters

David Ward ambaye ni mkurugenzi mkuu wa shirika huru la hisani la Taasisi ya FIA, amejiuzulu nafasi yake hiyo baada ya miaka 12, ili apambane dhidi ya Todt. Ward mwenye umri wa miaka 56, alisema kipindi cha uchaguzi kinaanza mwezi huu wa Septemba, na kwa hivyo ilikuwa muhimu kwake kuwafikia wanachama wa FIA ili aweze kupata uteuzi.

Todt alimrithi Max Mosley kama rais wa FIA mwaka 2009, baada ya kumshinda Ari Vatanen katika uchaguzi wa baraza kuu ya FIA, lakini Mfaransa huyo bado hajathibitisha iwapo anataka kugombea muhula wa pili baada ya muhula wake wa sasa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu. Ward anajivunia mtandao mkubwa wa kisiasa ndani ya FIA, unaotokana na nafasi yake ya zamani kama msaidizi wa Mosley.

Kimi Raikkonen.
Kimi Raikkonen.Picha: Reuters

Lotus yambembeleza Kimi Raikonnen

Na timu ya mashindano ya Lotus inafanya kila jitihada kumshawishi dereva Kimi Raikonnen abaki katika timu hiyo msimu ujao, mkuu wa timu hiyo yenye makao yake nchini Uingereza Eric Boullier amesema. Kumekuwa na minon'gono ya hapa na pale kuhusu mustakabali wa dereva huyo, raia wa Finnland mwenye umri wa miaka 33.

Wakati akisema anatumaini kuwa bingwa huyo wa dunia wa mwaka 2007 ataendelea kuwepo katika timu ya Lotus, Boullier alikri kuwa yapo masuala kadhaa yasiyopatiwa ufumbuzi, ambayo yanapaswa kushughulikiwa kabla ya kusaini mkataba mpya. Raikonnen yuko pointi 63 nyuma ya dereva anaeongoza katika ubingwa, Sebastian Vettel kutoka Ujerumani.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape, ap, afpe, rtre
Mhariri: Josephat Nyiro Charo