1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je,Fidel Castro bado ana usemi serikalini?

P.Martin1 Agosti 2008

Enzi ya Fidel Castro ilidhaniwa kuwa ilimalizika Julai 30 mwaka 2006,kiongozi huyo mgonjwa alipomkabidhi madaraka mdogo wake Raul Castro.

https://p.dw.com/p/EoGr
In this video frame grab image taken from the Cuban television program "Mesa Redonda" or "Round Table" which aired Tuesday June 5, 2007, provided by AP Television, Cuban leader Fidel Castro speaks during an interview from an undisclosed location in Cuba. Speaking slowly and focusing on past memories rather than his recovery and future, a healthier looking Castro gave the world its first long look at him since he fell ill and gave up power last summer. (AP Photo/AP Television)
Rais wa zamani wa Cuba,Fidel Castro.Picha: AP

Lakini miaka miwili baadae,yadhihirika kuwa Fidel Castro bado ana usemi nchini Cuba na kwa kiwango fulani,hata katika jukwaa la kimataifa.Ingawa Cuba haitawaliwi tena na Fidel Castro kama ilivyokuwa kwa takriban miaka 50,kiongozi huyo mwenye miaka 81 bado anasikilizwa na mdogo wake Raul Castro.Vile vile yeye huitumia kazi yake mpya aliyogundua kama muandishi wa makala maalum gazetini,kueleza maoni yake.

Katika duru za kidplomasia mjini Havana,kunaulizwa iwapo Fidel Castro anatumia ushawishi wake kuhakikisha kuwa Cuba inafuata sera zake za ujamaa na hivyo kuzuia mageuzi ya kiuchumi yanayopendelewa na mdogo wake.Lakini ndugu hao wawili wanasema,wao hawana ugomvi wo wote.

Lakini moja ni hakika:Fidel Castro amepata nafuu baada ya kusemekana kuwa alikuwa mahututi kufuatia upasuaji wa dharura wa utumbo uliofanywa Julai 2006 kwa ugonjwa uliowekwa siri.Alimkabidhi mdogo wake madaraka ya mpito na hakuonekana tena hadhrani isipokuwa katika kanda za video zilizoonyeshwa kwenye televisheni ya serikali.Katika kanda za mwanzo,Wacuba walishtushwa kuona jinsi alivyokuwa dhaifu.

Fidel Castro akajiuzulu rasmi kama rais katika mwezi wa February na hivyo kuliruhusu bunge la taifa kumchagua rasmi Raul Castro mwenye miaka 77 kama mrithi wake.Lakini badala ya kutoweka kama wengi walivyodhania,Fidel Castro ameibuka upya.Kwani katika mwezi wa Juni,baada ya kutoonekana kwa muda wa miezi mitano,kanda za video zilimuonyesha akiwa na afya na akikutana na Rais Hugo Chavez wa Venezuela na afisa wa Kichina He Guoqiang.

Vile vile akaanza kuandika makala maalum magazetini juu ya masuala mbali mbali;kuanzia Michezo ya Olimpiki hadi masuala ya kisiasa.Watu walioonana nae wanasema,afya yake imekuwa bora na akili zake ni timamu kabisa.Kuibuka kwake kumezusha minong'ono na kunaulizwa bado ana usemi gani serikalini.

Kwa upande mwingine,Raul Castro aliposhika wadhifa wa urais,alifanya mageuzi mbali mbali,kama vile kuwaruhusu Wacuba kununua simu za mkono na compyuta na hata kutumia hoteli na maeneo mengine ya burudani ambayo hapo awali yalikuwa kwa matumizi ya watalii tu.Vile vile akaondosha viwango vya mishahara ili kuhimiza uzalishaji na hata mamlaka ya uongozi katika sekta ya kilimo yaligawanywa idara mbali mbali.

Mageuzi katika sekta ya kilimo yaliendelea kwa kutoa ardhi zaidi kwa wakulima na mashirika binafsi.Lakini uhuru zaidi uliongojewa na wengi katika uchumi unaodhibitiwa na serikali haukutokea.Baadhi ya watu wanahisi Fidel Castro haungi mkono wazo la aina hiyo lakini wengine wanasema,rais huyo wa zamani hana usemi mkubwa hivyo na ni mambo mengine yanayochelewesha mageuzi.

Fidel Castro binafsi amesema,dhima yake ni ndogo tu.Amenukuliwa na vyombo vya habari vya serikali akieleza kuwa anachokifanya ni kukusanya habari na data na kuchambua matatizo ya kimataifa yaliyo na umuhimu mkubwa.Uchambuzi huo huwakilishwa kwa viongozi wa chama na taifa.

Kwa mujibu wa mchambuzi mmoja wa Kimarekani wa masuala ya kimataifa,ni dhahiri kuwa Fidel Castro bado ni mwanasiasa maarufu kabisa wa Cuba katika jukwaa la kimataifa,hata ikiwa siku hizi,chombo chake cha mawasiliano ni maneno yaliyoandikwa.