1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jenerali mpya achaguliwa kuongoza vikosi shirika nchini Irak

Hamidou, Oumilkher16 Septemba 2008

Jenerali Odierno,ashika nafasi ya jenerali Petraeus nchini Irak

https://p.dw.com/p/FJGJ
Waziri wa ulinzi Robert Gates amkabidhi hatamu za uongozi jenerali OdiernoPicha: AP



Jenerali Raymond Odierno amekabidhiwa hii leo hatamu za uongozi wa vikosi vya nchi shirika nchini Irak.Anashika nafasi ya jenerali David Petraeus anaesifiwa kwa kuimarisha usalama nchini Iraq.


Sherehe za kukabidhiwa hatamu za uongozi jenerali  Raymond Odierno,kutoka kwa msaidizi wake wa zamani jenerali David Petraeus zimefanyika leo mchana katika kasri la zamani la kiongozi wa zamani wa Irak Sadam Hussein,katika kituo cha kijeshi cha Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad.


Waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates aliyewasili Baghdad tangu jana,amembandika jenerali Odierno nishani ya nne,kuongoza wanajeshi laki moja na nusu wa nchi shirika-,ambao,asili mia 95 kati yao ni wa kutoka Marekani.


Jenerali Petraeus anaesifiwa kua chanzo cha kuimarika hali ya usalama tangu mwaka mmoja uliopita nchini Irak,amekabidhiwa jukumu la kusimamia opereshini za kijeshi katika eneo la mashariki ya kati na Asia ya kati.


Jenerali Petraeus amemsifu kiongozi huyo mpya wa vikosi vya nchi shirika akisema ni "mtu anaefaa kukabiliana na hali ya mambo ".


Waziri wa ulinzi Robert Gates amemsihi jenerali Odierno awe na subira,seuze tena mashambulio mawili yamefanyika jana na kugharimu maisha ya watu 34 nchini humo.


"Anajua tunajikuta njia panda ambapo maendeleo bado ni dhaifu na watu wanabidi kuwa na subira" amesema waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates.


Jenerali Odierno amekiri maendeleo yaliyopatikana ni dhaifu na hali ya mambo inaweza kubadilika.


Jenerali huyo ambae hii ni mara yake ya tatu kutumikia vikosi vya kimataifa nchini Irak anasema



"Nnaamini,la muhimu zaidi ni kuwa na serikali imara itakayoweza kumudu hali ya kisiasa ndani nchini Irak na katika daraja ya kimataifa.Kwa hivyo vikosi vya Irak vinatakiwa viwe  na ujuzi wa kutosha kuweza kutekeleza jukumu lao.Hapo tunaweza kupiga hatua mbele."



Jenerali Raymond Odierno alikua chanzo cha kugunduliwa Sadam Hussein mwishoni mwa mwaka 2003.Alilaumiwa sana hapo awali kwa kuamuru maguvu yatumike katika opereshini za kijeshi dhidi ya raia.



Hata kama mashambulio yamepungua nchini Irak,lakini mitihani kadhaa inamsubiri kiongozi mpya wa vikosi vya nchi shirika-mitihani inayoweza kukorofisha hali ya mambo.Mitihani hiyo ni pamoja na chaguzi za majimbo zilizopangwa kuitishwa mwishoni mwa mwaka huu au mapema mwakani na uchaguzi wa bunge  utakaofuatia mwishoni mwa mwaka 2009.


"Mtihani unaomkabili jenerali Odierno utahusiana na jinsi ya kushirikiana na wairak ili kuilinda hali ya mambo na kuieneza katika wakati ambapo vikosi vya Marekani vitapunguzwa" Ameonya waziri wa ulinzi wa marekani Robert Gates.


Majimbo 11 kati ya 18 yanadhibitiwa na vikosi vya jeshi la Irak na rais George w. Bush alisema wiki iliyopita,wanajeshi 8000 wa kimarekani watahamishwa hadi ifikapo mwezi January mwakani.