1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je,ni leseni ya kuishambulia Iran?

8 Julai 2009

Israel ni taifa huru na linaweza kuchukua hatua dhidi ya Iran inayohisi kuwa ni sahihi.Hayo alitamka Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden wakati wa mahojiano yake kwenye televisheni ya Marekani Jumapili iliyopita.

https://p.dw.com/p/IjtK
In this frame grab made from television, U.S. Vice President Joe Biden speaks to reporters aboard a C17 plane en route to Baghdad early Thursday July 2, 2009. (AP Photo/APTN)
Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden.Picha: AP

Wadadisi wametafsiri matamshi hayo ya Biden kama ni leseni iliyotolewa kwa Israel kuishambulia Iran. Na serikali ya Israel inayofuta sera za mrengo wa kulia na kuongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, imevutiwa na matamshi hayo ya ajabu ya Makamu wa Rais wa Marekani-leseni ya kuishambulia Iran. Hata serikali ya rais wa zamani wa Marekani George W.Bush ilijiepusha na suala hilo.Kwani mwaka mmoja uliopita, Bush na serikali yake waliiambia Israel wazi wazi kuwa Washington haina hamu ya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran. Serikali hiyo ilikwenda umbali wa kukataa kuipatia Israel silaha au kuiruhusu kupitia anga ya Iraq. Na sasa ni Mdemokrat Joe Biden alietoa idhini iliyokuwa ikingojewa kwa hamu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Avigdor Liebermann wala hakukawia kueleza maoni yake. Alisema:

"Naona kuwa amezungumza kimantiki. Taifa la Israel ni taifa huru. Hatimae ni serikali ya Israel ndio inayosimamia usalama na mustakabali wa nchi. Hata panapokuwepo tofauti za maoni kati ya washirika, maamuzi yetu mwishowe hupitishwa kwa kuzingatia maslahi ya kitaifa ya Israel."

Uhuru wa kijeshi unathaminiwa sana na serikali ya Israel. Mara kwa mara wanasiasa na vyombo vya habari nchini humo, kwa fahari hueleza hatua za kijeshi zilizochukuliwa na Israel binafsi, dhidi ya miradi ya nyuklia katika nchi jirani za Kiarabu. Kwa mfano shambulio la mwaka 1981 dhidi ya kituo cha nyuklia nchini Iraq, hutazamwa kama kitendo cha kishujaa. Na miaka miwili iliyopita, ndege za kijeshi za Israel zilishambulia kituo kilichoweza kuwa mtambo wa nyuklia nchini Syria-lakini shambulio hilo lilifanywa baada ya kushauriana na mshirika wake Marekani.

Wanasiasa katika serikali ya Israel wanasema, ikihitajika Israel itaishambulia Iran bila ya kujali maoni ya Washington. Na Makamu wa Waziri wa Mambo ya Nje Danny Aylon wa chama cha mrengo wa kulia amesisitiza kuwa Israel ni taifa huru na nchi hiyo, kamwe haikuomba idhini ya Marekani kuhusu operesheni au maamuzi ya kimkakati yanayohusika na Israel.

Lakini siku ya Jumanne, Rais wa Marekani Barack Obama katika mahojiano yake na CNN alisahihisha matamshi ya makamu wake Joe Biden. Obama alisema, Marekani wala haikutoa ruhusa kwa Israel kuishambulia Iran. Akasisitiza kuwa sera ya Marekani ni kusuluhisha mgogoro wa nyuklia wa Iran kupitia njia za kidiplomasia na kwa amani.

Mwandishi: S.Engelbrecht (ZPR) /P.Martin

Mhariri:Abdul-Rahman